Na Shamimu Nyaki


Kamati ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo leo Jijini Dodoma imepokea na kujadili taarifa ya Mfuko wa Utamaduni na Sanaa namna unavyotekeleza majukumu yake ya kuwaendeleza wadau wa sekta hizo.

Akiwasilisha taarifa kuhusu Mfuko huo kwa niaba ya Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana, Mtendaji Mkuu wa Mfuko huo Bi. Nyakaho Mahemba amesema hadi kufikia Agosti 2, 2023 kiasi Cha Shilingi Milioni 220,785,000/ kimerejeshwa kutoka kwa wanufaika wa mfuko huo ambayo ni sawa na asilimia 82 ya kiasi cha Shilingi milioni 269, 250,000/= zilizotakiwa kukusanywa kutoka kwa wanufaika 45.

"Mfuko wa Utamaduni na Sanaa umetoa mafunzo kwa Wadau 6,126 katika mikoa 11 na umezalisha ajira 88,725 pamoja na kuwezesha studio 21 kununua vifaa vya Kisasa vya kuzalisha kazi za Muziki na filamu" amesema Bi. Nyakaho.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Husna Sekiboko ameelekeza Wizara hiyo ihakikishe Mfuko huo unawanufaisha zaidi wasanii chipukizi na uzingatie pia mikoa yote kwa kuwa dhamira ya kuanzishwa kwake ni kuwafikia wasanii wote nchini.

Aidha, Wajumbe wa Kamati hiyo wameshauri mafunzo, mchakato wa kuwapata wanaopaswa kufaidika uwe wazi, vigezo na masharti yajulikane pamoja na mafunzo kwa wanufaika kuhusu namna ya kutumia mikopo hiyo kuendeleza kazi zao.

Akijibu hoja hizo Waziri Mhe. Balozi Pindi Chana amesema tayari Wizara imeshawasilisha maandiko ya miradi mbalimbali ya kuomba ufadhili wa kuchangia Mfuko huo ili uwe na mtaji mkubwa na uwezo wa kuwafikia na kuwanufaisha Wasanii wengi zaidi  akiongeza kuwa Mfuko huo utaendelea kuwasaidia  wadau wa Utamaduni na Sanaa kurasimisha kazi zao ikiwemo kuzisajili BASATA na Bodi ya Filamu.

Share To:

Post A Comment: