Na. WAF - Dar es Salaam.


Serikali kupitia Wizara ya Afya inafanya juhudi za kuhakikisha Hospitali zote Nchini zinakua na wodi maalum za uangalizi wa watoto njiti (NICU) na kushuka hadi katika ngazi ya jamii.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu leo akiwa katika ofisi ndogo za Wizara ya Afya Jijini Dar es Salam wakati wa maandalizi ya awamu ya pili ya kuendelea kugawa vifaa tiba katika Hospitali zenye wodi ya uangalizi maalum kwa watoto njiti (NICU).

“Tunataka Hospitali zote nchini ziwe na huduma za uangalizi maalum kwa watoto njiti na tunashuka hadi ngazi ya msingi kama vituo vya Afya kwakuwa 70% ya wanawake wajawazito wanajifungua katika Zahanati na Vituo vya Afya”, ameeleza Waziri Ummy

Aidha, Waziri Ummy amesema Rais wa JHamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa Tsh: Bil. 6.3 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba kwaajili ya kuanzisha wodi maalum kwa watoto njiti.

“Kwa kweli tunamshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia kwa kutupa fedha hizo na tayari tumeshanunua vifaa tiba, tumeanza kuvisambaza na tunaendelea kusambaza katika Hospitali zetu zaidi ya 80 nchi nzima”, ameweka wazi Waziri Ummy

Vile vile Waziri Ummy amewataka wanawake wajawazito wote nchini kuwahi katika vituo vya kutolea huduma za Afya, kupata huduma mapema ikiwa mjamzito anatatizo ili wataalamu waokoe maisha ya watoto na mama.

“Tunaweza kuokoa maisha ya watoto wetu wachanga na watoto njiti endapo mjamzito atawahi kupatiwa huduma mapema, kwa wakati na huduma sahihi”, amesisitiza Waziri Ummy

#TunaboreshaAfya
#MtuNiAfya
#JaliAfyaYako

Share To:

Post A Comment: