Watu 70 hufariki kila siku nchini Tanzania kutokana na Ugonjwa wa Kifua Kikuu (TB) na watu 25,800 hufariki kila mwaka kutokana na ugonjwa huo hapa nchini.


Hayo yameelezwa na Waziri wa Afya Ummy Mwalimu wakati akifungua Mkutano wa Makatibu Wakuu na Mameneja Mpango wa Programu za Kifua Kikuu kutoka Nchi 15 Barani Afrika unaofanyika kwa Siku Tatu Jijini Arusha.

Waziri Ummy amesema takwimu za kidunia zinaonesha kwamba takriban watu Milioni 10.5 wanaambukizwa ugonjwa wa Kifua Kikuu (TB) kila mwaka na kati yao watu takribani Milioni 1.6 hufariki kutokana na ugonjwa huo.

“Ikitokea basi la abiria limepata ajali na watu 70 wamekufa kila mtu ataandika Rest in Peace lakini Ugonjwa wa Kifua Kikuu unaua watu 70 kila Siku Tanzania ndio maana kwa kushirikiana na Mfuko wa Dunia wa kupambana na Kifua Kikuu, UKIMWI na Malaria (Global Fund) tumeamua kukutana na Makatibu Wakuu wa Wizara za Afya ili tujadili namna ya kuutokomeza ugonjwa huo ifikapo 2030”. Amesema Waziri Ummy.

“Takwimu zinaonesha kwamba takriban watu Mil. 10.5 wanaambukizwa ugonjwa wa Kifua Kikuu (TB) kila Mwaka Duniani na kati ya hao watu takriban Mil. 1.6 hufariki kutokana na ugonjwa huo”. Amesema Waziri Ummy

Pia, Waziri Ummy amebainisha kuwa kati ya Watu 100 watu 39 waliibuliwa na ugonjwa wa Kifua Kikuu kwa Mwaka 2015 nchini Tanzania ambapo hadi Sasa Serikali kupitia Wizara ya Afya imepiga hatua kwa kuweza kuibua wagonjwa hao kwa asilimia 65.

"Tumeongeza jitihada za kuendelea kuibua wagonjwa wa Kifua Kikuu kutoka Mwaka 2015 ambapo katika kila wagonjwa 100 tulibua wagonjwa 39 kwa Mwaka huo na kwa sasa tumeweza kuibua wagonjwa kwa asilimia 65 kwa kuwatumia wahudumu wa Afya ngazi ya Jamii". Amesema Waziri Ummy

Amesema, Jitihada hizo zimetokana na kuwatumia wahudumu wa Afya ngazi ya Jamii kwa sababu wao ndio wapo karibu na Jamii ambapo wanaweza kupita katika vilabu vya pombe, vijiweni, nyumba kwa nyumba pamoja waganga wa Tiba Asili baada ya kupewa mafunzo ya uelewa wa mgonjwa mwenye Kifua Kikuu.

Lengo la Mkutano huo ni kujadili kwa pamoja ni jinsi gani Nchi za Afrika zinaweza kuja na ubunifu pamoja na mikakati mipya ya kutokomeza Ugonjwa wa Kifua Kikuu Afrika na Duniani kwa ujumla ifikapo Mwaka 2030
.
Share To:

Post A Comment: