Katibu Mkuu wa CCK,Renatus Muabh.
Na Emmanuel Thobias
CHAMA Cha Kijamii (CCK) kimetahadharisha kuwa malumbano yanayoendelea kuhusu uwekezaji wa bandari ya Dar es Salaam hayana afya na yanaligawa taifa na hivyo kimeitaka serikali, Chama Cha Mapinduzi (CCM),vyama vya siasa vya upinzani na wadau wengine wazalendo kufikia muafaka wa kuruhusu maoni ya wananchi yafikie mwisho.
Katibu Mkuu wa CCK,Renatus Muabhi,katika taarifa
yake aliyoisambaza kwa vyombo vya habari leo (Julai 18, 2023),amesema ili
kufikia mwafaka wa suala hili kuna haja ya kuandaa mdahalo wa kitaifa ili
kutathimini msimamo wa serikali na maoni ya wananchi.
Muabhi alisema njia nyingine ya kufikia tamati
suala hili ni kuunda tume huru ya wadau itakayoshirikisha wajumbe kutoka
makundi tofauti yenye mawazo huru, kukusanya maoni na kutathimini msimamo wa
wananchi, jambo ambalo litaleta muafaka
na maridhiano kwa makundi yote yanayokinzana.
"Kikatiba mamlaka ya nchi yapo chini ya
wananchi, tutafute na tuelewe maoni ya wananchi yanataka nini na hofu yao ni
nini, hofu na mashaka yao vikiondolewa kwa kuridhiwa, tuanze utekelezaji wa
uwekezaji kwa kuwa hofu na mashaka vitakuwa vimetibika kwa mamlaka ya wananchi
wenyewe," alisema.
Muabhi aliongeza kuwa tusiruhusu kelele uchwara
za wachache wenye hila zao binafsi, kutaka kuburuza umma kwa tamaa zao za mali
jambo ambalo halitasaidia kumaliza mvutano huo.
" Wananchi wakionesha mashaka na kutoridhia,
tuachane mara moja na mkataba huu pamoja na hatua zake zote zinazopaswa kufuata
ili kuepusha serikali na chama tawala cha ccm, kutumia nguvu ya dola
kushinikiza jambo kwa wananchi," alisema Muabhi.
Alisema viongozi lazima watambue kuwa Serikali
iliyopo madarakani ni ya watu, iliwekwa na watu kwa ajili ya watu na
wanaipenda hivyo wanayomamlaka kisheria
kuikosoa bila kutishwa.
"Niwakati wa maridhiano, tukiri umoja wetu
umetikiswa, imani ya wananchi kwa serikali yao imetoweka, michuano hii ya hoja
inakoleza maswali kwa wananchi wasiojua mambo ya siasa na mikataba, ni wakati
wa maridiano," alisema.
Post A Comment: