Mbunge wa Singida Mjini, Musa Sima akiwahutubia Wananchi wa Kata ya Unyamikumbi iliyopo Manispaa ya Singida katika mkutano wa hadhara baada ya kutembelea na kukagua miradi ya maendeleo tisa iliyogharimu zaidi ya Sh.Bilioni 2 katika mkutano uliofanyika Julai 20, 2023.

..........................................................................

Na Dotto Mwaibale, Singida

MBUNGE wa Singida Mjini Musa Sima amemshukuru Mheshimiwa Rais, Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kupeleka fedha nyingi za miradi ya maendeleo kila sekta katika Kata ya Unyamikumbi ambapo zaidi ya Sh.Bilioni 2 zimetumika kutekeleza miradi hiyo.

Sima ametoa shukrani hizo jana Julai 20,  2023 alipokuwa  akielezea miradi iliyotekelezwa katika kata hiyo wakati wa muendelezo wa  ziara yake ya kutembelea na kukagua miradi hiyo pamoja na kufanya mkutano wa hadhara na kusikiliza kero za wananchi ili kuzitafutia ufumbuzi ambapo moja ya kero kubwa ni upungufu wa walimu,nyumba za kuishi pamoja na madarasa katika shule zilizopo pembezoni mwa manispaa hiyo na kuombwa kuifanyia kazi changamoto hiyo.

Katika ziara hiyo Sima aliambatana na wajumbe wa Kamati ya Siasa ya Wilaya ya Singida ambapo alisema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt Samia Suluhu imepeleka fedha nyingi katika kata hiyo kwa ajili ya miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa vyoo kwenye baadhi ya shule, ujenzi wa madarasa, miradi ya maji na ujenzi wa daraja lililopo Kijiji cha  Utamaha na kuwa lengo la Serikali kupeleka miradi hiyo ni kutoa huduma bora kwa wananchi.

Alisema katika utekelezaji wa miradi hiyo kupitia mfuko wa mbunge ametoa zaidi ya Sh.Milioni 10 kwenye maeneo tofauti ndani ya kata hiyo ili kusaidia ukamilishaji wa miradi hiyo.

Aidha, Sima ameipongeza na kuitaka timu nzima ya viongozi wa kata hiyo, wataalam na wananchi walioshirikiana kwa namna moja hama nyingine kuanzia mwanzo katika usimamizi wa miradi hiyo inayoendelea na kufikia hatua za mwisho kukamilika kuendeleza ushirikiano huo.

Mbunge Sima akizungumzia kuhusu mkataba wa Bandari ya Dar es Salaam dhidi ya Kampuni ya DP World ya Dubai alisema kuna mambo makubwa mawili Usalama na Biashara na kuwa Tanzania imeingia mkataba na kampuni hiyo kwa ajili ya kufanya biasharawa na si vinginevyo.

Aliwataka wananchi wa kata hiyo kuwapuuza wale wote wanaotaka kupotosha ukweli wa mkataba huo wenye tija kwa nchi yetu kuwa eti Rais Samia Suluhu Hassan ameiuza bandari hiyo.

Alisema wabunge wasingeweza kuridhia kufanyika kwa maridhiano ya mkataba huo baina ya Tanzania na DP World iwapo kama kungekuwepo kwa viashiria vya kuuzwa kwa bandari hiyo.

Alisema kupitia uwekezaji huo Tanzania itakuwa ikipata Sh.Trilioni 26 kwa mwaka tofauti na sasa ambapo tunapata Sh.Trilioni 7 tu kupitia bandari hiyo kwa mujibu wa taarifa zilizopo.

Alisema mkataba huo kwa kuzingatia sheria ya uwekezaji  ilipendekezwa kampuni hiyo isajiliwe Brela hapa nchini na iitwe  DP World Tanzania na wao wataingia mkataba na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) jambo ambalo litasaidia kusitisha mkataba huo kwa sheria za nchi yetu iwapo watashindwa kutimiza masharti na kuwa utahusisha Bandari ya Dar es Salaam tu na si na nyingine kama inavyopotoshwa.

Diwani wa Kata hiyo, Kipandwa Ipini alisema miradi iliyotembelewa na kukaguliwa na mbunge huyo jumla yake ni tisa na kuitaja pamoja na thamani yake kuwa ni ujenzi wa vyoo Shule ya Msingi Sundu ambavyo vimegharimu Sh.Milioni 18 ukiwepo na mchango wa wananchi.

Alitaja vyoo vingine kuwa ni vya Shule ya Msingi Ughaugha A vyenye matundu 12 ambavyo vimetumia Sh.Milioni 15 pamoja na michango ya wananchi huku Serikali ikitoa Sh.Milioni 11, madarasa ya Shule ya Msingi Unyamikumbi ambayo yametumia Sh.Milioni 19 ikiwa na michango ya wananchi ambapo Serikali ilichangia Sh.Milioni 15.

Alitaja mradi mwingine kuwa ni ujenzi wa madarasa manne yenye thamani ya Sh.Milioni 80, barabara ya Ughaugha na barabara ya Kihade jumla zimetumia Sh.Milioni 12 na kuwa ni barabara mpya ambazo zimefunguliwa kwa ajili ya kuharakisha maendeleo ya wananchi, ujenzi wa daraja la Kijiji cha Utamaha ambalo ujenzi wake umegharimu Sh.Milioni 98.4 na ujenzi wa madarasa mawili Shule ya Msingi Sundu yaliyogharimu Sh. Milioni 25 na madarasa mawili ya UVIKO 19 yenye thamani ya Sh.Milioni 40.

Alitaja kazi nyingine ni ujenzi wa maabara katika sShule ya Sekondari ya Unyamikumbi ambao ujenzi wake umegharimu Sh.Milioni 30 na kuwa jumla ya miradi iliyotekelezwa ina thamani ya Sh.Milioni 498,174,626.

Alisema miradi mingine ni ile ambayo bado inaendelea kutekelezwa kama ujenzi wa jengo la mama na mtoto unaojengwa katika Zahanati ya kata hiyo ambao mpaka sasa umetumia Sh.Milioni 5.8 ambapo hadi kukamilika kwake zitahitajika Sh.Milioni 148.5 na kutaja mradi mwingine ni ule wa kuboresha maji katika kata hiyo kutoka chanzo cha maji cha IRAO  ambao utagharimu Sh. Bilioni 1.3 na kuwa tayari umekwisha fanyiwa upembuzi yakinifu na kuwa fedha hizo zitafika wakati wowote kuanzia sasa.

Diwani wa kata hiyo hakumung’unya maneno wala kusita na kurudi nyuma ambapo naye alitumia nafasi hiyo kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuiona kata hiyo kwa jicho la huruma na kutoa kiasi hicho kkikubwa cha fedha kwa ajili ya kukamilisha miradi hiyo ambapo alimshuru pia Mbunge wa Singida Musa Sima, wataalam, viongozi mbalimbali na yeye mwenyewe kwa usimamizi mzuri uliotukuka wakati wa utekelezaji wa miradi hiyo.

Mbunge Sima akiwasalimia wanafunzi wa Shule ya Msingi Unyamikumbi wakati alipofika kukagua ujenzi wa madarasa mawili katika shule hiyo.
Mbunge Sima na Diwani wa Kata ya Unyamikumbi, Kipandwa Ipini wakikagua daraja lililojengwa katika Kijiji cha Utamaha kwa gharama ya Sh.Milioni 98.4.
Mbunge Sima akimkabidhi Sh. 100,000 Mwanafunzi wa Kidato cha nne, Happiness Athumani alizozitoa kusaidia kununua chakula kwa wanafunzi wa kidato hicho ambao wamepiga kambi ya masomo Shule ya Sekondari ya Unyamikumbi.
Mbunge Sima, akisalimiana na Mkuu wa Polisi wa Kata ya Unyamikumbi, Mkaguzi wa Polisi, Said Anyitike mara alipowasili kuanza ziara yake katika kata hiyo.Wananchi wa kata hiyo wamempongeza Anyitike kwa kufanya kazi kwa kujituma na kuwapa ushirikiano usiku na mchana pale wanapokuwa na changamoto mbalimbali ambazozinahusu huduma za kipolisi.
Mbunge Sima na Diwani wa Kata hiyo,, Ipini wakienda kukagua ukamilikaji wa ujenzi wa moja ya madarasa katika Shule ya Msingi, Unyamikumbi.
Mbunge Sima akizungumza na wanafunzi wa Shule ya Msingi Unyamikumbi.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi, Unyamikumbi, Julius Mgogo (kulia) akitoa taarifa ya ujenzi wa madarasa mawili katika shule hiyo.
Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Unyamikumbi, Shabani Mpinda akizungumza na wanafunzi wa shule hiyo.
Mkuu wa Jeshi la Polisi Kata ya Unyamikumbi, Mkaguzi wa Polisi, Said Anyitike akizungumza na wanafunzi wa shule hiyo ambapo aliwahimiza kufika kituo cha polisi kutoa taarifa za ukatili wa kijinsia iwapo watafanyiwa vitendo vya ukatili.
Diwani wa Kata hiyo Ipini akizungumza na wanafunzi hao.
Share To:

dotto mwaibale

Post A Comment: