Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mwanza na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja amekabidhi baiskeli tano zenye thamani ya shilingi milioni tatu kwa wananchi wenye ulemavu wa miguu Wilayani Sengerema na kuahidi kuwalipia bima ya afya, ikiwa ni mwendelezo  wa ziara yake ya kukutana na makundi maalum katika Jamii Mkoani Mwanza. 

Akizungumza katika mkutano wa hadhara katika eneo la Stendi ya zamani Mhe. Masanja amesema Serikali ya Awamu Sita inayoongozwa na Rais Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan imeweka mikakati ya kutatua changamoto za makundi maalum yasiyojiweza katika jamii hivyo msaada huo ni utekelezaji wa ilani ya CCM.

Mhe. Masanja amewaelekeza Madiwani na viongozi wengine wa Serikali kuibua wananchi wenye changamoto mbalimbali za ulemavu ili Serikali iwafikie na kuwasaidia.

"Kama kuna wananchi huko hawawezi kutembea wengine mmewaficha ndani, na kama kuna watoto wadogo hawawezi kwenda shule waleteni Serikali itawahudumia" Mhe. Masanja amesisitiza.

Aidha, Mhe. Masanja amewataka wananchi kuhakikisha wanaiunga mkono Serikali na kuipigia kura katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu unaokuja. 

Katika mkutano huo, Mhe. Masanja amesikiliza changamoto za baadhi ya wananchi kuhusu kero ya watumishi wa  maliasili kukamata baiskeli na pikipiki za wananchi, kero za maji, kero ya uhaba wa vifaa vya kujifungulia katika vituo vya afya,ardhi, uhaba wa walimu kero za  wafanyabiashara ndogondogo.

Mhe. Masanja ameahidi kuziwasilisha kero hizo katika Sekta husika na kufanyia kazi kero zinazohusu Sekta ya Maliasili na Utalii.

Share To:

Post A Comment: