Na. Damian Kunambi, Njombe


Baada ya kuishi pasipokuwa na umeme tangu kuumbwa kwa dunia kwa wakazi wa kijiji cha Mahorong'wa kilichopo katika kata ya Ludende wilayani Ludewa Mkoani Njombe hatimaye kijiji hicho kinakwenda kuwashiwa umeme ifikapo Agosti 5 mwaka huu.

Hayo yasemwa na mratibu wa miradi ya REA wilayani Ludewa mkoani Njombe Costansia Ndawela baada ya wananchi wa kijiji hicho kutoa kero ya kutowashiwa umeme huo mbele ya mbunge wa Jimbo la Ludewa Joseph Kamonga mara baada ya kufanya ziara katika kijiji hicho ikiwa ni mwendelezo wa wa ziara hiyo ya kutembelea vijiji vyote vya jimbo hilo. 

Bi. Ndawela ameongeza kuwa kwa sasa kila kitu kimekwisha kukamilika hivyo wanasubiri kufanyika kwa ukaguzi kati ya REA na TANESCO.

Kutokana na hatua hiyo iliyofikiwa mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga anawatoa hofu wananchi wa baadhi ya vitongoji na vijiji ambao bado hawajafikiwa na huduma hiyo, kuendelea kuwa wavumilivu kwani serikali bado inafanya jitihada ya kuhakikisha kila vijiji na vitongoji vinapatiwa umeme.

"Tutaendelea kuomba serikalini ili kila kitongoji kifikiwe na umeme, kwa mwaka huu wilaya yetu ya Ludewa imepewa vitongoji vipya 15 nje ya hivi vilivyopo sasa kwenye mpango ambavyo vitafikiwa na umeme hivyo tutaona namna ambavyo tunaweza kuleta na huku Ludende", Amesema Kamonga.

Aidha aliwataka wananchi hao kuwa na imani na serikali ya awamu ya sita kwani imedhamiria kusambaza umeme katika vitongoji vyote hapa nchini ikiwemo vitongoji vilivyopo pembezoni.

Mbunge huyo bado anaendelea na ziara hiyo ya kutembelea kijiji kwa kijiji huku akiwa ameambatana na viongozi wa chama cha mapinduzi ngazi ya wilaya hiyo na wakuu wa idara ambapo mpaka sasa tayari amekwisha tembelea vijiji 41 kati ya 77 vya jimbo hilo kwa lengo la kutoa mrejesho wa aliyoahidi na kupokea changamoto mbalimbali za wananchi

Share To:

Post A Comment: