MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Salim ASAS , ameushangaa ukimya wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Mkoa wa Iringa katika kutetea viongozi na mipango mbalimbali ya maendeleo inayofanywa na serikali ya chama chao likiwemo suala la uendeshaji wa Bandari lililoibua mjadala mkubwa hivi karibuni.

Akifungua Baraza la UVCCM la mkoa huu Asas amesema; “Kuwa wanachama wa UVCCM sio kuwa watu wa hamasa na kuimba tu, ni pamoja na kutimiza wajibu kusema mazuri ya chama na serikali yake, na kuwatetea viongozi wake dhidi ya kejeli na hujuma zinazofanywa na wapinzani.”

Akizungumzia makubaliano ya ushirikiano wa uendeshaji wa Bandari baina ya serikali ya Tanzania na Dubai, Asas alisema wapo baadhi ya watu kwa makusudi kabisa wamekuwa wakipotosha dhamira njema ya serikali katika mpango huo wakisema nchi inauzwa.

“Kuna vita ya kiuchumi na mnasikia kuna watu wanapotosha umma wakisema nchi inauzwa na ninyi vijana wetu mpo kimya tu. Hivi wanaosema nchi inauzwa wanajua thamani ya nchi hii kama sio lugha za kipuuzi tu?”alisema.

Akiwashangaa vijana kwa kushindwa kujibu hoja kama hizo alisema wakiendelea kufanya hivyo katika masuala nyeti na ya msingi inaweza kutoa tafsiri kwamba ukimya wao ni kwasababu wao pia wanaunga mkono upotoshaji unaoendelea.

“Lazima vijana wetu mjue kila unapofanya mema na mazuri ndipo unapozidi kupingwa. Jibuni hoja zao kwasababu hoja walizonazo zinajibika,” alisema na kuongeza kwamba ukiona hupingwi na badala yake unasifiwa tu ujue kuna mahali hufanyi vizuri.

Katika kujibu hoja za wapinzani hao wa maendeleo, Asas aliwataka vijana hao kutumia lugha za kistaarabu bila kutukana na watumie mitandao ya kijamii inayofikisha ujumbe kwa haraka badala ya kusubiri mikutano ya hadhara ambayo haiwezi kufanyika kila siku.

“Huko kwenye mitandao ya kijamii hatusikii kama kuna UVCCM, Rais na baadhi ya viongozi wanatukanwa na vijana wetu mliopa kulinda chama na viongozi wake mpo kimya, hatusikihi mkijibu hoja. Tambueni kazi yenu ni pamoja na kutetea chama ,viongozi wake na serikali yake,” alisema

Share To:

Post A Comment: