Na John Walter-Manyara

Wananchi katika mji wa Babati mkoani Manyara wameshtushwa kwa ongezeko la Bei ya Sukari ghafla bila taarifa.

Wakizungumza na kituo hiki leo Juni 27,2023 baadhi ya wananchi hao wamesema wanashangazwa kuona serikali ipo kimya juu ya suala hilo na kwamba ni siku ya pili leo bidhaa hiyo muhimu imepanda kutoka shilingi 2,800 kwa kilo moja hadi kufikia shilingi 4,000.

Wamesema hawajui sababu ya kupanda kwa bei hizo huku wakiiomba serikali iangalie suala hilo kwa kuwa maisha ni magumu.

Mmoja wananchi hao Ester Ruben amesema asubuhi ya leo amenunua sukari kwa shilingi elfu nne lakini wiki iliyopita alinunua kwa shilingi elfu mbili na mia nane.

Licha ya ongezeko hilo lakini pia katika maduka mbalimbali imekuwa ngumu kupatikana.

Mwenyekiti wa Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo (TCCIA) mkoa wa Manyara Musa Msuya, amekiri kuwepo kwa ongezeko hilo na kuongeza kuwa kuna baadhi ya wafanyabiashara wameficha sukari.

"Nafikiri watu wengi ni mashaka zaidi kwamba baada ya bajeti 2023-2024 kuanza kutumika kutakuwa na mfumuko wa bei, nahisi wameficha sukari  wakijua kuwa baada ya hapo watauza kwa bei ya juu" alisema Msuya

Mwenyekiti huyo amesema anaandaa mkutano utakaowakutanisha wafanyabiashara wenye maduka ya jumla ili kujua tatizo ni nini kwa sababu hakuna tamko lolote lililotolewa na serikali kuhusu kupanda kwa Bidhaa.


Share To:

Post A Comment: