Na. Damian Kunambi, Njombe.

Naibu  Katibu  Mkuu  Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira)  Dr. Sweetbert  Mkama ametembelea miradi mbalimbali ya uhifadhi mazingira inayotekelezwa katika halmashauri ya wilaya ya Ludewa mkoani Njombe sambamba na kukabidhi mashine za kufanyia kazi ikiwemo madhine ya kusagia chakula cha samaki yenye thamani ya Sh. Mil. 1.8.

 Katibu mkuu huyo ambaye aliambatana na Mratibu wa kitaifa wa mradi wa kuhifadhi ardhi katika bonde la ziwa Nyasa sambamba na Mkurugenzi wa halmashauri hiyo walikutana na vikundi vinavyoendesha miradi ya ufugaji nyuki, kuku pamoja na Samaki na kisha kukabidhi madhine hiyo ya kutengeneza chakula cha samaki ambayo inauwezo wa kusaga kilo 200 kwa siku.

Naibu katibu huyo amesema amevutiwa na mradi huo wa samaki kwani unaendeshwa vyema pasipo kuharibu mazingira na kuahidi kuwaletea mashine nyingine ya kutengeneza chakula ili waweze kuwa na uzalishaji mkubwa zaidi wa chakula cha samaki hao.

"Hiki kikundi kimenivutia sana, na ninapenda kuwaasa vijana wengine nao kuiga mfano wa hawa vijana. Lakini pia na nyie akina mama mnaofuga kuku nanyi endelezeni juhudi na wazee pia mnaofuga nyuki napenda niwapongeze pia na ninaahidi kuwaongezea mizinga 10 ili mfuge nyuki wengi zaidi".

Naye Mratibu wa kitaifa wa mradi wa kuhifadhi ardhi katika bonde la ziwa Nyasa Paul Deogratius amesema katika halmashauri hiyo ya Ludewa wametoa mashine ya kubangulia korosho, mashine ya kutotolesha vifaranga, Pamoja na mashine ya kusagia chakula cha samaki ili kuweza kurahisishia vikundi hivyo kufanya shuguli zao kwa urahisi.

Awali akisoma taarifa ya utekelezaji wa miradi hiyo Mkurugenzi wa halmashauri ya Ludewa Sunday Deogratias amesema halmashauri hiyo ilipokea kiasi cha zaidi ya sh. Mil. 85 ambazo zilipokelewa kwa awamu tatu na kuanzishwa miradi kwa kipindi cha mwezi Desemba 2017 hadi Aprili 2022 katika vijiji vya Mkongobaki, Kipangala, Ntumbati, Lupingu na Mdilidili ambapo naibu katibu mkuu huyo alifurahishwa na juhudi hizo na kukiri kuwa katika maeneo yote aliyopita hajakutana na maendeleo mazuri ya miradi kama ilivyo kwa Ludewa.

Deogratius aliongeza kuwa sambamba na kuanzishwa miradi hiyo lakini pia ilitolewa elimu ya uhifadhi mazingira kwa wananchi huku akieleza changamoto mabalimbali zinazowakabili.

" Ndugu Naibu katibu mkuu changamoto zilizopo ni baadhi ya wananchi kuwa na uelewa mdogo wa uhifadhi mazingira, ufinyu wa bajeti ya kuvifikia baadhi ya vijiji kutoa elimu, wakulima kukosa mitaji na kuongeza thamani ya mazao pamoja na miundombinu mibovu ya barabara na mawasiliano kwa baadhi ya vijiji".

Longnus Mgani ni mwenyekiti wa kikundi cha ufungaji samaki ametoa shukrani kwa niaba ya wenzake na kusema kuwa mashine hizo walizopewa ni chachu ya kuongezeka kwa uzalishaji wa mazao yao huku Diwani wa kata ya Lugarawa Erasto Mhagama akiwaasa wanavikundi hao kuzitunza mashine hizo walizopewa ili ziweze kuwasaidia kwa kipindi kirefu zaidi.

Share To:

Post A Comment: