Na Mohamed Saif

 

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Cyprian Luhemeja amewataka watumishi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA) kuhakikisha wanatumikia vyema nafasi zao walizoaminiwa  ili kuboresha hali ya upatikanaji wa huduma ya maji kwenye maeneo mbalimbali wanayohudumia.

 

Mhandisi Luhemeja ametoa maelekezo hayo kwa nyakati tofauti Juni 15, 2023 alipofanya ziara kwenye Ofisi mbalimbali za MWAUWASA ili kuzungumza na watumishi na kujadili changamoto zinazowakabili katika ufikishaji wa huduma ya majisafi na salama kwa wananchi lengo likiwa ni kuzipatia ufumbuzi wa pamoja na kuimarisha upatikanaji wa huduma ya maji Mwanza.

 

Ikiwa ni ziara yake ya kwanza Jijini Mwanza tangu ateuliwe kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Luhemeja alitembelea Ofisi zote za Kanda za MWAUWASA na kuzungumza na watumishi na kisha alihitimisha ziara yake kwenye Makao Makuu ya Mamkala hiyo katika jengo la Maji House kwa kukutana na watumishi wote.

 

"Ninaamini MWAUWASA mnao uwezo wa kufanya vizuri zaidi katika kuwahudumia wananchi, nina imani mkijipanga vyema hali ya huduma ya maji itaimarika," alisema Naibu Katibu Mkuu Luhemeja.

 

Alisema Jiji la Mwanza ni Jiji la Kimkakati na kwamba linahitaji kuwa na huduma bora na ya uhakika ya majisafi na salama hasa ikizingatiwa kuwa Serikali imewekeza fedha nyingi kuhakikisha huduma inaimarika.

 

"MWAUWASA ni Mamlaka ya Maji ya pili kwa ukubwa baada ya DAWASA, mpo kimkakati na Mkoa wa Mwanza ndio kitovu cha Kanda ya Ziwa na huu Mkoa unaakisi masuala yote ya kiuongozi Kanda ya Ziwa," alisisitiza Mhandisi Luhemeja.

 

Aidha, Mhandisi Luhemeja aliwaasa watumishi wa MWAUWASA kuhakikisha wanatanguliza mbele uzalendo, nidhamu, ubunifu, kuheshimiana na kufanya kazi kwa pamoja kwa maslahi mapana ya wananchi wanaowahudumia.

 

Mhandisi Luhemeja alisema Serikali imewaamini watendaji wa MWAUWASA na hivyo kuwapa dhamana ya kuwafikishia wananchi wa Mwanza huduma ya maji na aliwasisitiza kuhakikisha wanaienzi amana hiyo ili dhamira ya Serikali ifikiwe kikamilifu.

 

"Malalamiko ni mengi, hakikisheni mnajipanga vyema, mnasimamia kikamilifu usambazaji wa maji ili kufikisha huduma kote mnapopaswa kufikisha. Uzuri wa maji unaweza kuyahifadhi sio kama umeme kwahiyo mjitahidi wananchi yawafikie," ameelekeza Mhandisi Luhemeja.

Alisema upotevu wa maji ni mkubwa na aliielekeza Menejimenti ya MWAUWASA kuhakikisha inajipanga na inakuja na mikakati dhabiti ikiwa ni pamoja na kuishirikisha Wizara ya Maji katika harakati za kupunguza upotevu wa maji ili kuongeza upatikanaji wa maji wanayozalisha. 

 

"Ninawahakikishia sisi kama Wizara, chini ya uongozi wa Waziri wetu Mhe. Jumaa Aweso hatutawaangusha, tutaendelea kushirikiana nanyi kwa maslahi mapana ya wananchi ili dhamira ya Rais wetu mpendwa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kumtua Mama ndoo ya maji kichwani inafikiwa kikamilifu," alisisitiza Mhandisi Luhemeja.

 

Naibu Katibu Mkuu Mhandisi Cyprian Luhemeja anaendelea na ziara yake Mkoani Mwanza ya kukagua miradi ya maji inayoendelea kutekelezwa.

Share To:

Post A Comment: