Naibu Waziri wa Kilimo na Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini Mh. Anthony Mavunde amewataka wananchi wa Dodoma kujenga utamaduni wa kusafisha maeneo yao na kutunza mazingira ili kuendelea kulipendezesha Jiji la Dodoma.


Mavunde ameyasema hayo leo katika kata za Makole na Viwandani Jijini Dodoma aliposhiriki zoezi la usafi wa mazingira pamoja na wananchi wa Jiji La Dodoma ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya kuelekea kwenye kilele cha siku ya Mazingira Duniani.

“Nawashukuru wananchi wote mliojitokeza leo kushiriki katika zoezi la usafi wa mazingira katika Jiji letu la Dodoma.

Eneo letu limepata hadhi ya kuwa Mji mkuu wa Serikali hivyo lazima tulipe hadhi inayostahili hasa katika eneo hili la Mazingira,Mh Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan anafanya kazi kubwa sana ya kuliendeleza Jiji la Dodoma lazima na sisi tuwe mstari wa mbele kushirikiana nae kwa hali na mali.

Natoa rai kwa wanandodoma wote kujenga utamaduni wa kufanya usafi wa mazingira yetu na kutunza mazingira yetu kila wakati na sio tu wakati wa maadhimisho ya siku maalum kama hizi za leo”Alisema Mavunde

Akitoa maelezo ya awali Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Dkt. Sweetbert Mkama amesema zoezi hili la usafi la Jiji la Dodoma ni endelevu mpaka kufikia siku ya Kilele cha Maadhimisho ya siku ya Mazingira Duniani tarehe 5 Juni 2023 ambapo Mgeni Rasmi anatarajiwa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh Dkt . Philip Isdor Mpango na kutumia fursa kuwataka wakazi wa Jiji la Dodoma kushiriki kwa wingi katika tukio hilo kubwa la mazingira.Share To:

Post A Comment: