Raisa Said,Tanga


Uelewa wa jamii juu ya masuala ya malezi ya watoto hasa wenye umri wa miaka 0-8 umeelezwa kuwa jambo muhimu katika kuirejesha jamii katika mstari wa malezi sahihi ya watoto nchini Tanzania.

Hayo yameelezwa na Katibu Tawala Mkoa wa Tanga, Pili Mnyema alipotembelewa na timu ya Mtoto Kwanza wanaotekeleza Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT-MMMAM) 2021/22- 2025/2926 kwa mkoa huo kwa ajili ya kujitambulisha rasmi ofisini kwake .

Timu hiyo iliongozwa na Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Tanga, Glory Maleo,
Raisa Said mwandishi wa Gazeti la Mwananchi na Kinara wa Habari za Watoto, Regis Temba kutoka United Help for Tanzania Children (UHTC), Dk Samwel Mturu pia kutoka UHTC.

Mnyema alisema kuwa suala la uelewa wa jamii ni muhimu sana katika malezi ya watoto kwa sababu jamii ikielewa basi malezi ya watoto yatakuwa katika mstari unaotakiwa.

“Kwa mfano wakati sisi tukiwa tunakua, jirani anaweza akamkemea mtoto wa mwenzake akiona anafanya makosa. lakini siku hizi haiwezekani. Mtu anaweza akaona kabisa mtoto wa mwenzake anapotea lakini yeye atasema kwani ni mtoto wangu,” alisema Mnyema.

“Ingawa jukumu la malezi linaaanzia kwa mzazi lakini jamii nzima inatakiwa kuwa na uelewa sahihi juu ya maelezi ya mtoto,” alisema na kueleza kuwa siku hizi kutokana na wazazi kujishughulisha sana na masuala ya kutafuta fedha jukumu la malezi limeachwa kwa walimu hivyo alisema kuwa kuna kazi kubwa ya kuwapa elimu wanajamii juu ya malezi sahihi.

Alisisitiza juu ya umuhimu wa ushirikiano na akawasihi waandishi wa habari na vyombo vya habari kwa ujumla kuendelea kuandika na kuelimisha jamii juu ya malezi ya watoto kwa sababu mambo yao yanafika haraka kwa jamii.

Aliwahakikishia wajumbe wa timu hiyo ushirikiano kutoka kwa viongozi wote katika halmashauri zote na kusema viongozi wa ngazi mbalimbali katika wilaya hizo ndio walio karibu zaidi na wananchi.

Programu Jumuishi ya Kitaifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto ilizinduliwa Dodoma na aliyekuwa waziri wa Afya kipindi kile Dk Dorothy Gwajima kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hasaan mwaka 2021.

Wanaotekeleza programu hiyo ni timu ya Mtoto Kwanza, Mtandao wa Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali Tanzania(TECDEN)  (TECDEN), Children in Crossfire (CIC) na Vilabu vya waandishi wa Habari Tanzania( UTPC )na Serikali kwa ujumla.


Share To:

Post A Comment: