KITUO cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC), kimejipanga kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi tatu bora Afrika katika kupokea watalii wa mikutano kutoka nafasi ya tano kwa sasa.

Kwa mujibu wa Chama cha Kimataifa Vituo vya Kimataifa vya Mikutano Duniani (ICCA), Tanzania ipo nafasi ya tano katika idadi ya watalii wa mikutano ya kimataifa Afrika ambayo ni asilimia 10 ya soko la mikutano yote ya kimataifa inayofanyika Afrika.

Mkurugenzi Mwendeshaji wa AICC, Ephraim Mafuru alisema ili kuhakikisha Tanzania inafanya vizuri katika medani za utalii wa mkutano Afrika, AICC imedhamiria kuboresha miundombinu yake kwa kumbi za kisasa za mikutano ya kimataifa, hoteli za hadhi ya nyota tano, maduka makubwa, benki pamoja na viwanja vya michezo na burudani jijini Arusha.

“Tumedhamiria kujenga mji wa kisasa katika eneo la ekari 90.8 na kuipaisha Tanzania na jiji la Arusha kuwa siyo tu kuwa sehemu maarufu kwa utalii wa Mikutano bali pia nchi ya kila aina ya michezo na burudani,” alisema.

Mafuru alisema AICC itajenga kituo cha Kimataifa cha Mikutano kitakachojulikana kama “Kituo cha kimataifa cha Mikutano Kilimanjaro” katika eneo hilohilo lilipo eneo la D1 na E lilipo kijenge unapoelekea barabara ya Njiro.

Aidha, aligusia mpango mwingine wa kujenga mji mwingine wa Kisasa utakaohusisha kituo cha Kimataifa cha mikutano, benki, viwanja vya michezo na maduka makubwa katika jiji la Unguja na baadaye Dodoma.

Share To:

Post A Comment: