Bertha Mollel, Arusha

Waziri wa Maliasili na Utalii mh. Mohamed Mchengerwa anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa maonyesho ya Kimataifa ya utalii ya Karibu-  KiliFair yatakayofanyika katika viwanja vya Magereza jijini Arusha kuanzia Juni 2 hadi 4 mwaka huu.

Katika maonyesho hayo ya kila mwaka, kampuni zaidi ya 370 za utalii kutoka nchi 12 duniani wanatarajiwa kushiriki kuonyesha bidhaa zao kwa wanunuzi kutoka mataifa 38 duniani zilizothibitisha kuhudhuria.

Akizungumzia maandalizi ya maonyesho hayo, Mkurugenzi wa Kampuni ya Kilifair Promotion, ambao ndiyo mwandaaji mwenza wa maonyesho hayo, Dominic Shoo, amesema maandalizi yote yamekamilika.

Shoo amesema kuwa wanunuzi hao watatembelea vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo hapa nchini ambayo ni fursa ya nchi kuendelea kutangaza vivutio vya utalii kwa wageni kutoka mataifa makubwa ya kitalii duniani.

"Kupitia onyesho hilo tunalofanya kila mwaka tumefanikiwa kuleta watu zaidi ya 500 kutoka mataifa mbalimbali duniani ambao tunaamini wamekua mabalozi wazuri wa  kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini,"alisema Shoo

Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wakala wa Utalii Tanzania (TATO), Henry Kimambo amesema lengo la kukutanisha wadau wa utalii wa ndani na nje ya nchi ni kufanikisha azma ya serikali ya kufikisha watalii milioni tano ifikapo mwaka 2025.

Kwa upande wake afisa mtendaji mkuu wa bank ya CRDB Boma Rabilla ambaye alikabidhi hundi ya milioni 50 ikiwa ni sehemu ya mchango wa kufanikisha maonyesho hayo amesema kuna haja ya kuunga mkono jitihada zozote za kuongeza watalii.

"Ikitoka biashara ya dhahabu iliyoingiza Bilioni 2.8 za kimarekani inayofuata ni sekta ya utalii iliyoingiza Bilioni 2.4 hivyo kufanikisha maonyesho haya ni kufanikisha kuongeza fedha za kigeni nchini" amesema Rabilla.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Ndege Tanzania (ATLC), Patrick Ndekana, alisema wataendelea kutoa mchango wa kuchagiza sekta mbalimbali za kiuchumi ikiwemo ya utalii.

"Kwa sasa soko la China limefunguka na sisi tunaenda kule mara tatu kwa wiki,hivyo hii ni fursa kwetu sisi wadau wa utalii kuliangalia hili soko kwa jicho la karibu sana,maonyesho haya yawe chachu ya kufungua na kuvutia watalii toka China,"amesema

Share To:

Post A Comment: