WAZIRI wa Kilimo, Hussein Bashe amesema Tanzania inajitosheleza kwenye hazina ya chakula na pia baki ya kuuza nje.

Ameyasema hayo leo Mei 8,2023 akiwasilisha bajeti ya wizara hiyo bungeni mjini Dodoma na kusema kuwa uzalishaji wa mazao ya chakula katika mwaka 2021/2022 ilikuwa  tani Milioni 17.14, ambapo mahitaji ya
chakula kwa mwaka 2022/2023 ni tani milioni 15.05.

Amesema makadirio ya mahitaji ya chakula ifikapo mwaka 2030 yatakuwa tani milioni 20 na mwaka 2050 yatakuwa tani milioni 33.7.

” Hali hii inaleta changamoto kwa nchi yetu kuwa na mikakati ya uwekezaji ya muda mrefu kwenye sekta ya kilimo ili kuhakikisha utoshelevu wa chakula kwa miaka hiyo na ziada kwa ajili ya kuuza nje ya nchi, ” amesema

Aidha, amesema mchango wa kilimo katika uchumi kwa mwaka 2021 ilikua kwa asilimia 3.9 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 4.9 mwaka 2020.

Vilevile, Sekta ya Kilimo imechangia asilimia 26.1 katika Pato la Taifa; imetoa ajira kwa wananchi kwa wastani wa
asilimia 65.6 na kuchangia asilimia 65 ya malighafi za viwanda na asilimia 100 ya chakula nchini.

“Ninapenda kulitaarifu Bunge lako Tukufu kwamba, kwa mwenendo wa ukuaji wa idadi ya watu
ndani ya nchi na duniani ifikapo mwaka 2050, nchi yetu itakuwa na idadi ya watu milioni 136 na dunia itakuwa na watu bilioni 9.7.

“Katika kipindi hicho, uzalishaji wa chakula duniani unakadiriwa kupungua kwa asilimia 4 wakati mahitaji halisi ya chakula yanakadiriwa kuongezeka kwa zaidi ya asilimia 50,” amesema.

Share To:

Post A Comment: