Rais wa Shirikisho la Vyama Vya Wachimbaji Madini Tanzania ( FEMATA) John Bina (katikati) akizungumza na Wajumbe wa Kamati ya Utendaji wa shirikisho hilo katika kikao cha siku mbili kilicho anza leo May 27, 2023, Ukumbi wa Hotel ya Aqua Mjini Singida ambacho kitafikia tamati kesho. Kulia ni mgeni rasmi wa kikao hicho Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Singida, Chone Malembo na kushoto ni Mwenyekiti wa Wanawake wachimbaji madini Taifa, Martha Kayaga.
...........................................................
Na Dotto Mwaibale, Singida
SHIRIKISHO la Vyama vya Wachimba Madini Tanzania (FEMATA) linatarajia
kuanzisha benki yao ambayo itatumika kuwakopesha wachimbaji kwa lengo la kuinua
sekta hiyo muhimu kiuchumi nchini.
Hayo yamesemwa na Rais wa FEMATA,
John Bina wakati akizungumza katika kikao cha siku mbili cha Kamati
Tendaji ya shirikisho hilo ambacho
kimeanza leo May 27, 2023 na kufikia tamati kesho May 28, 2023 chenye lengo la kukamilisha mchakato wa
kuandika katiba mpya ambayo itaendana na wakati wa sasa pamoja na kujadili
mambo mengine.
Bina alisema wamefikia hatua ya kuanzisha benki hiyo kwa ajili ya
kuwasaidia wachimbaji ili waweze kukopeshwa fedha za mitaji ya kuendesha
shughuli za uchimbaji baada ya kuwepo changamoto za kukopeshwa fedha na mabenki
yaliyopo hapa nchini.
"Wachimbaji tumekuwa na changamoto kubwa katika sekta yetu hii muhimu
katika kuinua uchumi wa nchi, tumekuwa tukitumia zana duni na kufanya kazi kwa
kiwango cha chini kutokana na kuwa na mitaji midogo na kibaya zaidi hata
tukienda katika mabenki yaliyopo kuomba mkopo tumekuwa hatukopeki ndio maana
tukaona ni vizuri tukaanzisha ya kwetu," alisema Bina.
Alisema ili shirikisho hilo liendelee kuwa imara ni lazima liwe na katiba
inayoendana na wakati wa sasa, baadae, wakati uliopo na ujao.
Alisema FEMATA ilianzishwa mwaka 1986 na katiba inayotumika ni ya tangu
mwaka huo hivyo wamekubaliana katika vikao tofauti na kufikia maazimio hayo
kwenye kikao walicho keti Musoma mkoani Mara na Tanga ambapo imeendelea
kuandikwa na sasa wamefika mwisho wa kupata katiba hiyo.
Katika hatua nyingine Bina alitumia nafasi hiyo kuwahamasisha wananchi wa
Mkoa wa Singida kuchangamkia fursa ya uchimbaji wa madini mengi ya aina
mbalimbali yaliyopo mkoani hapa.
"Singida ina akiba ya madini ya kutosha lakini changamoto iliyopo ni
ya rasilimali watu mimi kwetu ni hapa Singida lazima niwaambie acheni uzembe
fanyeni kazi wenzetu wasukuma ndio wanaofanya kazi ya uchimbaji wa madini
katika migodi iliyopo, dhahabu iliyoyopo Geita inaweza kuwa ni nyingi lakini
Singida inaweza kuwa nyingi zaidi shida
hapa ni rasilimali watu sisi wanaSingida tumekalia kubishana badala ya kufanya
kazi," alisema Bina.
Bina aliwaomba viongozi wa vyama vya wachimba madimi Mkoa wa Singida
kuwaeleza wananchi umuhimu wa madini na faida zake jambo litakalowasaidia
kuamka na kuanza kufanya kazi hiyo ikiwa pamoja na kupata ajira na kuinua
maisha yao kiuchumi badala ya kuwaachia fursa hiyo ichangamkiwe na watu wengine
kutoka nje ya mkoa huo.
Aidha, Bina alizungumzia tozo wanazotozwa wachimbaji kwenye Halmshauri za
Wilaya wanapotunga sheria wawe wanawashirikisha viongozi wa FEMATA kwani zimekuwa nyingi na kuwa kero kwao.
Alisema changamoto nyingine iliyopo ni Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)
kuja na mfumo wa kuwatoza kodi kwa asilimia mbili wakati wao wana asilimia saba
na kwamba hawakatai kulipa kodi kwani kulipa kodi ndio msingi wa maendeleo na
kuiomba mamlaka hiyo iangalie namna ya kuiondoa kodi hiyo ambayo imekuwa kero.
Bina aliomba TRA wakae pamoja na wachimbaji
kujadili kodi hiyo iliyoanza kutozwa ili kuona namna bora ya kuliweka
sawa jambo hilo pasipo kuumiza upande wowote.
Afisa Mkazi wa Madini Mkoa wa Singida, Chone Malembo, ambaye alikuwa mgeni
rasmi, alisema katiba iliyopo imeweza kuwafikisha hapo walipo lakini katibu
mpya kwa sasa ni ya muhimu kwani itasaidia kuwapeleka mbele zaidi na kujibu
changamoto mbalimbali zilizokuwa zikijitokeza mwanzo.
"Hivi sasa dunia imebadilika ikiwa ni pamoja na sekta yenyewe hivyo
naamini katiba mpya italeta tija na maendeleo sambamba na kuondoa changamoto
mlizokuwa mkikabiliana nazo," alisema Chone.
Aidha, Chone aliomba shirikisho hilo kufungua milango ya kuwaita wachimbaji wengine kutoka mikoa mingine kuja kuwekeza mkoani Singida kwani Tanzania ni yetu sote.
Afisa Madini Mkazi, Mkoa wa Singida, Chone Malembo akitoa hutuba yake ya ufunguzi wa kikao hicho. |
Naibu Katibu Mkuu FEMATA, Peter Kabepela, akizungumza katika kikao hicho. |
Mhazini Mkuu wa FEMATA, Gregory Kibusi, akizungumza kwenye kikao hicho. Katibu wa Wachimbaji wadogo Mkoa wa Singida, Innocent Makomelo, akizungumza kwenye kikao hicho |
Post A Comment: