NA FARIDA MANGUBE MOROGORO.


Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Prof. Raphael  Chibunda amesema kukamilika kwa Jengo  Mtambuka la Mafunzo limetatua changamoto ya vyumba vya kufundishia na kujifunzia katika Kampasi  Kuu ya Edward Moringe Sokoine.

Prof. Chibunda ameyasema hayo kwenye hafla  fupi ya kuwapongeza wafanyakazi waliofanya vizuri kwa kipindi cha mwaka moja  ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha kilele cha siku ya wafanyakazi Duniani ambapo kitaifa kimefanyika mkoani Morogoro .

Amesema jengo hilo linauwezo wa kuchukua  wanafunzi zaidi ya elfu tatu kwa mara moja, ofisi  za wafanyakazi pamoja na maabara ambapo Chuo kimemuomba Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kuweza kulizindua jengo hilo.

“Tumemuomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kama itapendeza aje atuzindulie jengo hili japo tumeshaanza kulitumia.” Alisema Prof. Chibunda

Aidha amesema kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) SUA imepokea kiasi cha shilingi Bil.73.6 ambazo ni sawa na Dola za kimarekani Milioni 32 ambazo zimegawanywa kutumika katika makundi mawili ambayo Bil. 55.2 zitatumika Kampasi Kuu ya Edward Moringe na kiasi cha shilingi milioni 18.4 kitatumika Kampasi yao ya Katavi kwa lengo la kuboresha elimu kwa Chuo hicho.

Amesema kupitua HEET walimu 43 kutoka SUA wamepata fursa ya udhamini wa kujiendeleza kimasomo katika vyuo mbalimba nje ya nchi lengo likiwa ni kuboresha elimu inayotolewa kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu.

Kwa upande wake katibu na mratibu wa Mei Mosi kutoka  SUA, akisoma risala kwa Makamu mkuu wa Chuo ameuomba uongozi wa Chuo kutatua kwa wakati changamoto za wafanyakazi ikiwemo kupandishwa kwa madaraja kwa wenye sifa hizo.

Pia ameomba kutocheleshwa kulipwa kwa stahiki mbalimbali za wafanyakazi kama vile nauli za mizigo, posho za kujikimu na malimbikizo yanayotokana na mabadiliko ya miundo ya utumishi.Share To:

Post A Comment: