Na John Walter-Manyara

Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Paulina Gekul amewataka wananchi kutumia Huduma ya msaada wa kisheria ya Mama Samia (Samia Legal Aid Campaign), kupata haki zao na kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia.

Naibu Waziri Gekul ametoa wito huo leo mei 23,2023 mjini Babati wakati akizindua kampeni hiyo kwa Mkoa wa Manyara, itakayotolewa bure kwa wananchi wote kwa siku kumi katika wilaya tano za mkoa huo.

Amesema kampeni hiyo inayosimamiwa na serikali kupitia wizara ya Katiba na Sheria, itasadia kuimarisha mfumo wa utoaji Huduma za msaada wa kisheria kuanzia Serikali Kuu Hadi Serikali za Mitaa.

Pia, Gekul amewaagiza viongozi wote kuanzia ngazi ya Vijiji, kuweka mfumo mzuri wa kushighilikia changamoto za kisheria zitakazoibuliwa wakati wa kampeni hiyo.

Aidha amesema wataalamu wa sheria kutoka wizara ya Katiba na Sheria watakuwepo katika wilaya zote tano za mkoa wa Manyara kwenye majimbo Saba kuwasikiliza wananchi kuanzia ngazi ya kata na kutoa elimu ya masuala mbalimbali yanayohusu Sheria.

Kampeni hiyo inayotekelezwa chini ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa kushirikiana na Shirika la Legal Services Facility (LSF) na mashirika mengine, imepewa jina la Samia, ili kuenzi mchango wa Rais Dr. Samia Suluhu Hassan katika kutokomeza vitendo vya ukatili hasa kwa kina mama, watoto na makundi Maalum na kutoa nafasi ya msaada wa kisheria bure kwa wananchi wote.

Mwakilishi wa mkuu wa mkoa wa Manyara Kheri James  ambaye ni mkuu wa wilaya ya Mbulu, amesema mkoa upo tayari kutoa ushirikiano ili wananchi waweze kupata huduma hiyo muhimu.

Mwenyekiti wa chama cha Mapinduzi Pater Toima amempongeza na kumshukuru Rais kwa kuwakumbuka wanyonge wanaokosa haki zao kwa kutokujua sheria.

Share To:

Post A Comment: