Upakiaji kwenye pikipiki watoto wa shule walio chini ya umri wa miaka minane unahatarisha afya na usalama wao.
Vyombo mbadala vya usafiri kama bajaj inashauriwa kutumika kwa ajili ya kusafirisha wanafunzi walio chini ya umri wa miaka minane kutokana na kuwa bora zaidi kwa usalama wa watoto hao.

Na Abby Nkungu, Singida

ELIMU duni katika jamii juu ya Sheria za usalama barabarani na umasikini wa kipato  vimetajwa kuwa  miongoni mwa sababu za baadhi ya wazazi na walezi kuwasafirisha watoto wao wa chini ya miaka 8 kwa kutumia pikipiki maarufu kama "bodaboda" wakati wa kwenda shule na kurudi nyumbani, jambo ambalo ni hatari kiafya na linahatarisha usalama na ulinzi wa kundi hilo muhimu.

Hayo yalibainishwa na Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani cha Jeshi la Polisi mkoa wa Singida, Nestory Ndidi wakati akizungumzia mafanikio na changamoto za utekelezaji wa Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto  iliyoanza Januari 2021/2022.

Alisema kuwa licha ya Programu hiyo inayoendelea hadi 2025/2026 kuleta mabadiliko chanya katika jamii  kwa kutatua changamoto za Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (MMMAM); ikiwemo ulinzi na usalama wao, suala la wanafunzi wadogo kupakiwa kwenye pikipiki limeachwa zaidi kusimamiwa na kikosi cha usalama barabarani licha ya kuwa ni hatari na linagusa wadau wengi.

“Naam, sisi ndio Wasimamizi wa Sheria za usalama barabarani ambapo inakatazwa kumpakia kwenye pikipiki mtoto aliye chini ya miaka 9, ili kulinda usalama na afya yake na hii ni kwa mujibu wa Sheria ya Wakala wa kudhibiti Usafirishaji wa Ardhini (LATRA) iliyoanzishwa 2010 na kuanza kufanya kazi rasmi 2011 ambapo vyombo hivyo vya usafiri vilivyoingia kwa wingi nchini na kuanza kusafirisha abiria” alisema Ndidi

Alifafanua kuwa kutokana na wingi wa bodaboda karibu kila sehemu nchini, LATRA nao wamekasimisha madaraka hayo kwa halmashauri za Miji, Majiji na Manispaa ili kusaidia usimamizi wake, lakini kwa kiasi kikubwa  suala hilo limeachwa kwa Jeshi la Polisi  kitengo cha usalama barabarani.

Hata hivyo, alisema kuwa katika kusimamia sheria hiyo wanalazimika kutumia busara zaidi kutokana na ukweli kwamba kila wanapotaka kumsimamisha dereva wa bodaboda naye huongeza mwendo; hivyo kuacha kuendelea kumfukuza; hasa anapokuwa amepakia mtoto au watoto kwani anaweza kupata ajali kwa mwendo kasi na kusababisha hatari zaidi kwa afya, ulinzi na usalama wa mtoto.

Alisema kuwa kupitia utekelezaji wa Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto ipo haja kwa  wadau wote; wakiwemo wazazi, walezi, walimu na mamlaka zingine kuunganisha nguvu ili kukomesha suala la watoto wa chini ya miaka  8 kupakiwa kwenye pikipiki jambo ambalo sio tu ni kinyume cha sheria bali pia ni hatari kwa afya ya mtoto.

Kaimu Mganga Mkuu wa Manispaa ya Singida, Dk. Hamisi Yuna alisema kuwa kiafya mtoto anayebebwa kwenye pikipiki bila kuwa na nguo nzito za kumsitiri baridi na upepo njiani anaweza kupata magonjwa ya njia ya hewa ambayo tiba yake inaweza kugharimu fedha nyingi.

"Taarifa ya magonjwa  yanayowakumba watu wenye umri wa miaka 5 na kuendelea katika Manispaa yetu kwa Januari hadi Machi mwaka huu, inaonesha magonjwa ya njia ya hewa ndio yanayoongoza kutokana na jumla ya watu 8,572; wakiwemo watoto wa miaka 5 kuathirika, hiyo ikiwa ni sawa na asilimia 22" alifafanua na kuongeza;

"Hivyo, natoa wito kwa wazazi na walezi kuangalia uwezekano wa kuanza kutumia usafiri mwingine  mbadala; kama vile bajaj kwa watoto wa chini ya miaka minane ili kulinda afya  na usalama wao".

Baadhi ya wazazi na walezi wanasema elimu duni kwa jamii juu ya Sheria za usalama barabarani na umasikini wa kipato ndio sababu za kutumia bodaboda kupeleka watoto shule na kuwarudisha nyumbani.

“Mimi nilikuwa sijui kabisaaa kuwa sheria inazuia bodaboda kubabe watoto ndio kwanza nasikia hapa kwako, lakini pia angalieni na kipato basi wazazi wengine hawawezi kumudu gharama za mabasi ya shule maana hiyo tu buku ya kwenda na buku nyingine ya kurudi nyumbani yaani 2000/- kwa siku zinatutoa jasho hali ni ngumu” alisema Shabani Ali mmoja wa wazazi mkazi wa Minga Singida mjini. 

Kauli hiyo imeungwa mkono na Neema Daniel mkazi wa Mtipa ambaye anasema ingawa baadhi ya wazazi wanatambua hatari licha ya sheria lakini tatizo ni uwezo wa kifedha ndio maana wanaamua kutumia pikipiki huku wakimuomba Mungu apishe mbali mabaya yote.

“Watoto wanaamka asubuhi sana kuna wakati anapakiwa kwenye pikipiki huku akiwa bado na usingizi, ni hatari akilala bado anapigwa na upepo ambao pia ni mbaya kwa afya yake, lakini hakuna namna zaidi ya kuomba Mungu tu. Kikubwa, mamlaka husika kuendelea kutoa elimu kwa jamii juu ya madhara ya kiafya na kiusalama yanayoweza kumkumba mtoto anayetumia pikipiki kila mara" alieleza.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo asilimia 43 ya watoto wapo kwenye hatari ya kutofikia hatua timilifu za ukuaji kutokana na viashiria kama vile utapiamlo, umasikini na kukosekana kwa uhakika wa  chakula.  

Share To:

dotto mwaibale

Post A Comment: