Na Mapuli Misalaba, Shinyanga

Watu wawili wamefariki Dunia katika matukio mawili tofauti yaliyotokea Mkoani Shinyanga hivi karibuni.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga kamishna msaidizi wa Polisi Leonard Nyandahu wakati akizungumza na Misalaba Blog amewataja watu hao kuwa ni TUMAINI MALIMA mwenye umri wa miaka 35 mkazi wa mtaa wa Kambarage Manispaa ya Shinyanga na mwanaume mwingine anayekadiliwa kuwa na umri wa miaka 35 mpaka 40 ambaye hakufahamika jina na makazi yake.

Amesema TUMAINI MALIMA amefariki Dunia akiwa anapatiwa matibabu Hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Shinyanga Mwawaza baada ya kujeruhiwa kwa kupigwa jiwe na Yohana Daniel akiwa Bar ya Heinken mjini Shinyanga.

Kaimu Kamanda Nyandahu amethibitisha kifo cha mtu wa pili   anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 35 – 40 ambaye hakufahamika jina wala makazi yake  ameuawa kwa kushambuliwa na wananchi kwa tuhuma za kuiba Mahindi mabichi shambani katika kijiji cha Mwamalili kilichopo Manispaa ya Shinyanga.

Kaimu Kamanda wa Jeshi la polisi Mkoa wa Shinyanga Leonard Nyandahu ametoa wito kwa wananchi kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi na badala yake kutoa taarifa kwa jeshi la polisi pindi matukio ya uhalifu yanapotokea.

Share To:

Misalaba

Post A Comment: