MWENGE wa Uhuru Kitaifa 2023 umeendelea na ziara yake katika wilaya ya Songea mkoani Ruvuma ambapo Aprili 19,2023 umekagua na kuridhia miradi yote katika Halmashauri ya Madaba.


Miongoni mwa miradi iliyoridhiwa na Mwenge wa Uhuru ni mradi wa ujenzi wa maji katika Kijiji cha Mbangamawe ambapo serikali kupitia RUWASA imetoa zaidi ya shilingi milioni 545 kutekeleza mradi huo.

Akitoa taarifa ya mradi huo kwa Kiongozi wa Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2023 ,Meneja wa RUWASA Wilaya ya Songea Mhandisi Mathias Charles amesema mradi huo ukikamilika kwa asilimia 100 utawawezesha wakazi 2,800 kupata maji safi na salama ya bomba.

Akizungumza baada ya kukagua mradi huo,Kiongozi wa Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2023 Ndugu Abdalla Shaib Kaim amewapongeza RUWASA kwa kuendelea kutekeleza miradi ya maji yenye viwango vinavyoendana na thamani ya fedha zilizotolewa na serikali.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Songea Mheshimiwa Kapenjama Ndile kwa niaba ya wananchi amemshukuru Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha zilizowezesha kujenga mradi wa maji katika Kijiji cha Mbangmawe ambacho hakijawahi kuwa na maji ya bomba tangu kuanzishwa kwake.

Miradi mingine ambayo imetembelewa na Mwenge wa Uhuru katika Halmashauri ya Madaba ni mradi wa lishe katika zahanati ya Likarangilo na mradi wa mapambano dhidi ya dawa za kulevya katika Kijiji cha Magingo.

Mwenge wa Uhuru pia ulikagua mradi wa utunzaji mazingira na kutembelea chanzo cha maji katika hifadhi ya misitu ya Wino inayosimamiwa na Wakala wa Misitu Tanzania (TFS),ambapo Kiongozi wa
Mwenge wa Uhuru amepongeza kazi kubwa inayofanywa na TFS kwenye
utunzaji mazingira nchini.

Katika Halmashauri ya Madaba pia Mwenge wa Uhuru umeweka jiwe la msingi kwenye mradi wa nyumba ya kulala wageni katika Kijiji cha Lilondo iliyojengwa na Mwananchi binafsi Ibrahimu Kilangwa kwa gharama ya shilingi milioni 126.

Kiongozi wa Mwenge wa Uhuru Kitaifa katika Halmashauri ya Madaba pia ameweka jiwe la msingi katika kikundi cha Kwetu Madaba ambacho

kimepewa mkopo na Halmashauri shilingi milioni 44 kufanya mradi wa kufyatua tofali za saruji.

Mwenge wa Uhuru pia umekagua na kufungua rasmi vyumba viwili vya madarasa vyenye thamani ya shilingi milioni 40 katika sekondari Madaba.

Kulia ni Kiongozi wa Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2023 Ndugu Abdalla Shaib Kaim akifurahi baada ya kuweka jiwe la msingi mradi wa maji katika kijiji cha Mbangamawe Halmashauri ya Madaba wilayani Songea mkoani Ruvuma ambapo serikali imetoa shilingi milioni 545 kutekeleza mradi huo kupitia RUWASA.
Mradi wa maji katika kijiji cha Mbangamawe Halmashauri ya Madaba wilayani Songea mkoani Ruvuma unatekelezwa na RUWASA ambapo serikali imetoa shilingi milioni 545 kutekeleza mradi huo wenye uwezo wa kuhudumia wakazi 2,800,Mwenge wa Uhuru umeridhia kuweka jiwe la msingi kwenye mradi huo
Katikati ni Meneja wa shamba la Windo Madaba wilayani Songea Mhidadhi Grory Kasmiri akitoa taarifa ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania TFS katika shamba la Wino kwa kiongozi wa Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2023 Ndugu Abdlalla Shaib Kaim 
Share To:

Post A Comment: