Vijana Nchini wametakiwa kuwa na tabia ya kusoma historia za waasisi wa Zanzibar ili kuleta mawazo chanya yatakayojenga Taifa la baadae.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla ametoa wito huo akifungua Kongamano la Tano la kumbukumbu ya Marehemu Sheikh Abeid Aman Karume lililoandaliwa na Chuo cha kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Kampasi ya Karume Bububu Zanzibar.

Amesema kujua historia ya Zanzibar na Waasisi wake kutasaidia kupata maarifa ya namna ya kufanyakazi kwa mashirikiano katika jamii na Taifa kwa ujumla na hatimaye kufikia hatua kubwa za maendeleo.

Mhe. Hemed amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inachukua hatua mbali mbali za kuwaletea maendeleo wananchi wake katika sekta ya Kijamii, kiuchumi na kisiasa kwa kuzingatia misingi iliyowekwa na kiongozi shupavu Marehemu Mzee Abeid Aman Karume ya kuwaunganisha wazanzibari na watanzania kwa ujumla kwa kuimarisha ustawi wa jamii na kuharakisha maendeleo.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameeleza kuwa ni miaka hamsini na Moja (51) tokea kuuwawa kwa Marehemu Sheikh Abeid Aman Karume bado fikra, mawazo na maono yake yanaenziwa kivitendo kwa kuamini kuwa ndio chachu ya maendeleo endelevu ya Zanzibar.

Ameeleza kuwa Serikali ya Awamu ya Nane inayoongozwa na Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi itaendelea kusimamia fikra za waasisi hao kwa lengo la kuwaletea maendeleo wananchi wake kupitia Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2020 – 2025.

Aidha Mhe. Hemed amefurahishwa kuona Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere kinaishi na falsafa ya kuwaenzi waasisi wa Taifa la Tanzania kwa vitendo ikiwa pamoja na kufanya makongamano ili jamii itambue umuhimu wa mchango wa waasisi katika ujenzi wa Taifa.

Sambamba na hayo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameupongeza Uongozi wa Chuo hicho kwa kuwa na mtaala wenye fani mbali mbali zinazoendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia ambazo zimewawezesha wanafunzi kuwa na ubunifu utakaorahisisha upatikanaji wa huduma bora kwa jamii.

Pamoja na hayo Mhe. Hemed ameeleza kuwa kuanzishwa kwa mashindano ya uandishi wa Insha kunatoa fursa kwa wanafunzi wa Skuli za Msingi na Sekondari kujifunza na kujua historia za waasisi wa taifa letu na kuwajenga katika misingi ya kuipenda nchi yao.

Aidha ametoa wito kwa jamii ma Taifa kwa ujumla kuiga mfano huo wa ushirikishwaji wa watoto na kutowaacha nyuma katika mambo yanyowajengea uzalendo katika Taifa lao.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo cha kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Mhe. Stephen Masato Wasira ameeleza kuwa juhudi za kiukombizi za Mzee Karume zimeanza kabla ya Mapinduzi baada ya kuanzishwa kwa Chama cha Afro Shirazo Party (ASP) 1957katika kupigania uhuru wa Afrika.

Aidha ameipongeza Serikali ya Awamu ya Nane kwa kuendeleza fikra na maono ya muasisi huyo katika kukuza Uchumi wake.

Nae Mkuu wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Profesa Shadrack Sakai Mwakalila ameeleza kuwa lengo la kuandaliwa Kongamano hilo ni kuwakutanisha wanataaluma na wanajamii kutathmini shughuli mbali mbali za kijamii kwa kusimamia kauli na Fikra za Viongozi waasisi wa Taifa la Tanzania.

Katika Kongamano hilo mada mbali mbali zimewasislishwa ikiwemo Mchango wa Marehemu Sheikh Abeid Aman Karume katika uboreshaji wa huduma za Afya na Elimu katika Zanzibar ya leo ambayo imewasilishwa Dkt. Zaria Mohamed Abubakar na Mtazamo wa Marehemu Sheikh Abeid Aman Karume katika kujenga Misingi ya ushirikishwaji kijinsia kuelekea uchumi wa buluu Zanzibar iliyowasilishwa na Mhe. Juma Hassan Reli.

Awali Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alikagua maonesho kujionea vipaji na ubunifu mbali mbali vilivyowasilishwa na wanafunzi wa Chuo cha kumbumbu ya Mwalimu Nyerere.






Share To:

Post A Comment: