Na Shua Ndereka,Dodoma

WADAU wa Haki ya Kupata Habari (CoRI), wameshauriwa kujipanga kwa hoja na mifano pale watakapokutana na wabunge kwa ajili ya kutoa ufafanuzi kuhusu mabadiliko ya sheria ya habari wanayoyataka.


Kauli hiyo ilitolewa na Faustine Ndungulile, Mbunge wa Kigamboni wakati alipokutana na wadau hao kuzungumzia baadhi ya vipengele vilivyoachwa katika muswada wa habari.


Serikali ilipeleka muswada huo bungeni na kusomwa kwa mara ya kwanza tarehe 10 Februri 2023, ambapo unatarajiwa kujadiliwa katika Bunge hili la bajeti ama la Septemba mwaka huu.


Akizungumza na Neville Meena, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji TEF pia Deus Kibamba ambaye ni Mjumbe wa CoRI, Ndungulile alisema, ujenzi wa hoja imara utashawishi wabunge.


“Muwe na ufafanuzi halisi na unaoweza kushawishi wabunge, tena kwa mifano; Mfano mnataka kusiwepo na leseni, je nchi nyingine zinafanyaje hasa za Afrika.


“Kila hoja mnayoitoa iwe na ufafanuzi mzuri kwa wabunge, mkifanya hivyo, mnaweza kushawishi wabunge na jambo linaweza kuwa rahisi,” alisema.



Cosato Chumi, Mbunge wa Mafinga alisema, sheria zetu zinapaswa kuendana na mabadiliko makubwa ya teknolojia, vinginevyo zinaweza kuwepo lakini hazitekelezeki.


Chumo alitoa kauli hiyo baada ya Deodatus Balile, Mwenyekiti wa TEF alipoeleza madhara ya kuwa na sheria za habari zinazoshusha taswira Tanzania kimataifa.


Balile alisema, kuwa na sheria inayokataza kuingia kwa machapisho ya nje bila kuweka vigezo halisi, kunasababisha taifa kuingia kwenye orodha ya mataifa yanayonyonga uhuru wa habari.


“Kuwa na sheria kama hii tena inayompa mwanya waziri kuamua kuzuia machapisho kwa namna anavyojisikia, kunaweza kusababisha hata machapisho yenye umuhimu kutoka nje hata kama yana faida na nchi, kuzuiwa.


“Tunaamini kuna machaposho yanapaswa kuzuiwa lakini vigezo viwekwe wazi, kutokuweka wazi kunatoa taswira hasi, lakini katika ulimwengu huu wa teknolojia, unawezaje kuzuia machapisho wakati muda wote yapo kwenye simu?” Balile alihoji.


Mbunge Cosato alisema, kulingana na dunia ilipo sasa, ni vizuri bunge kutunga sheria zinazoendana na mazingira ili ziweze kutekelezeka.


“Ninaelewa mantiki ya hili, sioni kama sheria ya kuzuia machapisho inaweza kufanya kazi kwa wakati huu tulionao kwani muda wote machapisho yapo mkononi (kwenye simu). Sheria za namna hii zifanyiwe kazi,” alisema.


Hata hivyo, alisema hoja ya sheria kutoweka ukomo wa kiwango cha chini cha adhabu ya kifungo ina mashiko; “kweli ukiweka kiwango cha chini cha adhabu, maana yake unamlazimisha hakimu atoe adhabu ya kifungo, si kila kosa linahitaji kifungo.”


Akizungumzia utaratibu wa utoaji wa wa leseni kwa magazeti, Nusrat Henje ambaye ni Mbunge wa Viti Maalum alisema, sheria inampa mwanya mtoa leseni (Habari Maelezo) kuamua nini cha kufanya kwa chombo cha habari husika.


“Wakati mwingine serikali inaweza kuamka na ‘stress’ na ikaja na maamuzi ambayo sio. Ni vizuri vyombo vya habari mambo yao yakawa yanafanyika kwenye bodi yao,” alisema.


Mbunge huyo alisema, kuna kila sababu kwa tasnia ya habari kuwa na sheria rafiki ili kutoa fursa kwa ujenzi bora wa taifa.


“Ninaona hoja zenu na umuhimu wake, sisi kama wabunge tutashauri kamati namna bora ya kuliendea hili. Tunatamani kuwa na sheria zinazoishi muda mrefu, si hivyo tu bali zinazotekelezeka,” alisema.


Judith Kapinga, Mbunge wa Viti Maalum alisema, kuna baadhi ya vipengele muhimu vya sheria ya habari vimeachwa na kwamba, kwa ufafanuzi uliotolewa na CoRI unashaiwshi kujumuishwa kwenye sheria ijayo.
Share To:

OKULY BLOG

Post A Comment: