Na Denis Chambi, Tanga.

WAFANYABIASHARA   wa vyakula katika masoko ya Mgandini na Ngamiani  yaliyopo ndani ya Halmashauri ya jiji la Tanga wamelia na changamoto mbalimbali zinazowakabili ikiwemo  miundombinu mibovu iliyopo licha ya ushuru wanaotozwa hali ambayo inachangia kuharibika kwa bidhaa zao kabla ya kuuza.

Wakizungumza mbele ya mwenyekiti wa chama cha mapinduzi mkoa wa Tanga Rajab Abdurlahman March 29,2023 katika ziara yake ya kutembelea,  kujua upatikanaji wa bidhaa na  hali ya bei ilivyo hususani kipindi hiki katika masoko hayo walisema kuwa pamoja na  bidhaa kupatikana  na wastani na  bei kuwa ya kawaida  bado  uchakavu wa miundo mbinu imekuwa ni tatizo sugu kwao licha ya viongozi na  serikali kutoa ahadi za mara kwa mara  kuwawekea mazingira rafiki.

Katibu wa soko la Mgandini  Shabani Mohammedi alisema kuwa licha ya wafanyabiashara waliopo katika soko hilo kuchangia shilingi elfu tisa kila mwezi kulingana na maelekezo ya halmashauri ya jiji la Tanga lakini bado hawaoni  faida yake kutokana na kuendelea kufanya baishara zao katika mazingira magumu hasa kayika nyakati za mvua.

"Tuna kilio cha muda mrefu cha kujengewa soko tunalipa ushuru kama kawaida na hakuna mfanyabiashara aliyekataa n tumekuwa tukiahidiwa muda mrefu kujengewa soko lakini halijengwi ,  ukiachana na hilo kuna malori yanayoingia hapa ni mengi ambayo yanaweza kusaidia kuwezesha kuchangia mapato kwa kulipia ushuru " alisema Mohammed.

Mmoja wa wafanyabiashara wanaouza viazi katika soko la Mgandini alisema kuwa bidhaa hiyo ambayo wamekuwa wakiipata nje ya mmoa wa Tanga  wamekuwa wakikutana na changamoto ya usafiri wakitozwa ushuru kuwa mkubwa kila mahali wanapopita  kabla ya kufika sokoni hapo  wakiwa  na hayimaye kuambulia tu hasara.

"Wateja kipindi hiki cha Ramadhani sio wengi kivile tunakutana na changamoto njiani wakati tunasafirisha mzigo  kutoka shambani hasa sisi wa viazi serikali ijue kwamba sisi hatupati faida tunapata hasara  tunatozwa ushuru mkubwa njiani na tukifika hapa sokoni  viazi  vinaoza"

Akizungumza mara baada ya kujionea hali ya upatikanaji wa bidhaa,  bei  na miundombinu ilivyo katika  masoko yote  mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi 'CCM' Mkoa wa Tanga Rajab  Abdulrahman alisema kuwa wamejipanga kufanya ziara katika masoko yote yaliyopo mkoani humo kwa lengo la kujua changamoto wanazokutana nazo wafanyabiashara na kuona namna nzuri ya kuweza kuzitatua kwa manufaa ya wananchi wote.

" Ziara yetu ya leo tumekuja kuangalia hali ya upatikanaji wa bidhaa pamoja na hali ya bei zake lakini nitarudi sasa maalum baada ya mwezi mtukufu wa Ramadhani  kufanya ziara mkoa mzima wa Tanga na ikiwemo katika mji wa Tanga wenyewe na katika soko hili la Mgandini ndio hasa pana changamoto kubwa  soko hili mmeahidiwa kwa muda mrefu na  halijengwi miundombinu yake  ya hovyo hivyo lazima miundombinu ikae katika hali nzuri ili mraji wa mwisho aweze kufaidika apate matunda ya nchi yake" alisema Rajab.

"Nitafanya ziara mahususi katika mkoa mzima wa Tanga kila halmashauri  watueleze wamejipangaje kuondoa kilio cha muda mrefu cha wafanyabiashara kuwaboreshea miundo mbinu katika mazingira yaliyo mazuri maana mwisho wa siku ukimboreshea mfanyabiashara unafanya afya ya mlaji nayo iweze kuimarika lakini sio katika hali iliyopo sasa haitulidhishi tunaamini serikali itafanyia kazi ushauri ambao tunatoa" aliongeza.

Hata hivyo licha ya kipindi hiki cha mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani  ambapo  awali ilizoeleka kuwa bei za bidhaa na vyakula vingi kupanda lakini katika masoko hayo bei ipo kawaida kama siku zote huku bidhaa zikitajwa kuadimika kutokana na kipindi cha ukame wa baadhi ya maeneo hii ikichangiwa na ukosefu wa mvua za kutosha.
 
 
 
Mwenyekiti wa chama cha Mapinduzi 'CCM' Mkoa wa Tanga Rajab Abdulrahman akizungumza na mmoja wa wafanyabiashara wa Nyama  waliopo katika soko la Ngamiani jijini Tanga wakati alipofanya ziara yake ya kutembelea masoko kujua hali ya upatikanaji wa bidhaa na bei zake katika kipindi hiki cha  mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani  jumatano.

Mwenyekiti wa chama cha Mapinduzi 'CCM' Mkoa wa Tanga Rajab Abdulrahman akizungumza na mmoja wa wafanyabiashara wa vyakula  waliopo katika soko la Mgandini lililopo jijini Tanga wakati alipofanya ziara yake ya kutembelea masoko kujua hali ya upatikanaji wa bidhaa na bei zake katika kipindi hiki cha  mfungo wa mwezi mtukufu aa Ramadhani juzi jumatano.Picha na Denis Chambi Tanga.
Share To:

Post A Comment: