Wanafunzi wenye Ualbino wanahitaji zana bora za kujifunzia tangu wakiwa madarasa ya awali na msingi ili kuwa na msingi bora wa elimu.
Na Abby Nkungu, Singida
SERIKALI imeombwa kuangalia uwezekano wa kuboresha mazingira ya kujifunzia
na kufundishia pamoja na kuweka miundombinu yote muhimu kwa watoto wenye
mahitaji maalum katika shule zake za awali na msingi ili kuwezesha kutekelezeka
kwa vitendo Sera ya elimu Jumuishi.
Chini ya Sera ya elimu Jumuishi ya mwaka 2014, watoto wenye ulemavu, wenye
mahitaji maalumu na walio kwenye mazingira magumu wanatakiwa kusoma na wenzao
wa kawaida kwenye shule moja bila kubaguliwa ili kila mtoto wa Kitanzania apate
haki ya elimu bila kikwazo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya wadau wa elimu wanasema licha
ya Sera hiyo kuwa mkombozi; hasa kwa watoto wasio na uwezo ambao awali walikuwa wakifichwa majumbani kutokana
na wazazi au walezi wao kushindwa kuwapeleka kwenye shule maalumu, changamoto
ya kutokuwepo kwa mazingira rafiki kwenye shule Jumuishi bado ni kikwazo
kingine.
Mkurugenzi wa Shirika lisilo la Kiserikali linaloshughulikia maendeleo ya
elimu Mtinko (MEDO), Iddi Hashim anasema kabla ya Sera ya elimu Jumuishi wazazi
na walezi wa watoto wenye ulemavu na mahitaji maalumu walikuwa wakilazimika kutafuta shule maalumu; ambazo
hata hivyo ni chache.
“Sera hii imesaidia hasa kwa watoto wa chini ya miaka 8 maana shule Jumuishi zipo jirani. Mzazi au mlezi
anaweza kumpeleka mtoto wake wa awali,
darasa la kwanza au la pili shule mapema asubuhi kisha jioni akaenda kumchukua
na kumrejesha nyumbani" anasema Iddi Hashim.
Hata hivyo, Iddi anasema changamoto
kubwa iliyobaki hivi sasa ni kwa Serikali kuongeza bajeti kwa shule hizo ili
ziweze kuboresha mazingira ya kujifunzia na
kufundishia pamoja na kuweka miundombinu wezeshi kwa watoto wenye
ulemavu na wenye mahitaji maalumu kusoma bila kikwazo.
“Hata wewe ungekuwa mzazi usingekubali kupeleka mtoto wako anatembea kwa
mkono kwenye shule ambayo haina choo maalumu au mlemavu wa miguu kusikokuwa
na ngazi mtelezo au basi pale Mtinko tulivyoona mtoto asiyeeona kwenye
mtihani analazimika kusubiri mwenzake anayeoona amalize kwanza ndipo aanze
kumsomea yeye” alisema na kuiomba
Serikali kuangalia suala hilo.
Anasema kuwa ingawa Serikali hivi sasa imekuwa ikihakikisha shule mpya za
msingi zinakuwa na ngazi mtelezo na vyoo kwa wenye mahitaji maalumu, majengo ya
zamani bado ni kikwazo, uhaba wa walimu wa elimu maalumu na zana za kujifunzia
na kufundishia kama vile maandishi ya
nukta nundu, lugha ya alama, miwani kwa wenye uoni hafifu na mengine
mengi.
Mmoja wa wazazi ambaye ni Afisa Maendeleo ya Jamii mstaafu, Patrick Mdachi
anasema kuwa ingawa Sera ya elimu Jumuishi imesaidia; hasa watoto wadogo
wasioweza kutembea umbali mrefu kufuata
shule za vitengo maalumu lakini bado kuna umuhimu kwa Serikali kuongeza bajeti
ili ziweze kutekeleza kwa vitendo Sera hiyo na kuleta manufaa yaliyokusudiwa.
“Programu Jumuishi ya Taifa juu ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya
Mtoto ( PJT-MMMAM) iliyoanza Januari mwaka 2021 na inaendelea, inaangalia zaidi
suala la elimu, afya, lishe, ulinzi na usalama wa mtoto; hivyo ni vizuri
na hii
Sera ikawekewa mazingira mazuri ili iweze kutekelezeka vyema” alisema na
kuongeza kuwa lengo ni mtoto mwenye mahitaji maalumu kupata elimu bila kikwazo.
Msisitizo wa wazazi wengine, akiwemo Daudi Lameck mkazi wa Mtipa,
Kulwa Ali wa SIDO na Neema Daniel wa
Sabasaba ni kwa Serikali kuboresha zaidi shule zinazotekeleza Sera hiyo ili
kuvutia watoto hao.
“Zamani, wazazi na walezi tulikuwa tunawaficha hawa watoto majumbani ili
wasisome, sio kwa kupenda bali tulikuwa tukiona akienda shuleni ni kama
atateseka zaidi kulingana na mazingira yasiyo rafiki huko kuliko kubaki
nyumbani lakini sasa hivi tunawatoa wakasome.....Serikali itusaidie kuweka
mazingira mazuri” anasema Neema huku akiungwa mkono na Daudi pamoja na
Kulwa.
Takwimu za halmashauri ya Manispaa ya Singida zinaonesha kuwa jumla ya watoto 84 wenye
mahitaji maalumu wamesajili kwenye shule na vitengo mbalimbali kuanza masomo ya
awali na msingi mwaka huu 2023 ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 30
ikilinganishwa na mwaka jana 2022.
Afisa elimu msingi katika Manispaa hiyo, Omary Maje anasema pamoja na
sababu nyingine, mafanikio hayo ya uandikishaji watoto wenye mahitaji maalumu
yametokana na utekelezaji mzuri wa Programu Jumuishi ya Taifa juu ya Malezi,
Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto ya mwaka 2021.
Maje anasema chini ya Programu hiyo, pamoja na mambo mengine ya usalama, ulinzi, makuzi, afya, lishe na masuala mengine mengi mtambuka, viongozi na watendaji wa mitaa wamekuwa wakizunguka kwenye maeneo yao kuwabaini watoto hao na kutoa elimu juu ya umuhimu wa kupewa elimu.
Zana bora za kujifunzia kama hii anayotumia kijana huyu ni muhimu kwa watu wenye uoni hafifu.
Mfano wa choo bora kwa ajili ya matumizi ya wenye mahitaji maalumu pamoja na wengine wasio na mahitaji maalum.
Post A Comment: