Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba akizungumza na wadau wa Sekta ya Afya wakati akifungua mafunzo ya wawezeshaji wa Mfumo Mshitiri kutoka Halmashauri Saba za mkoa huo katika mkutano uliofanyika mjini hapa Machi 30, 2023. Kushoto ni Mganga Mkuu wa Mkoa wa Singida, Victorina Ludovick na kulia ni  Mwezeshaji wa kitaifa wa mfumo huo kutoka Wizara ya TAMISEMI, Emmanuel Mayunga,

Na Dotto Mwaibale, Singida

MKOA  wa Singida umeendelea kujidhatiti na kuongeza ufanisi katika upatikanaji wa huduma bora za afya kwa kutekeleza afua mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutumia mfumo wa Mshitiri kwa bidhaa za afya zinazokosekana Bohari ya Dawa (MSD).

Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba wakati akifungua mafunzo ya wawezeshaji wa Mfumo Mshitiri kutoka Halmashauri Saba za mkoa huo ambazo ni Itigi, Iramba, Singida Manispaa, Ikungi, Manyoni, Singida DC na Mkalama.

“Kutokana na changamoto na kuibuka kwa hoja mbalimbali za ununuzi wa bidhaa za afya vituoni, Ofisi ya  Rais - TAMISEMI ilitoa waraka namba moja wa mwaka 2018 ambao ulielekeza matumizi ya washitiri teule wa mikoa katika ununuzi wa bidhaa za afya pale vituo vinapokosa bidhaa kutoka MSD,” alisema.

Serukamba alisema kuwa uwapo wa mfumo huo ni utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 kama ilivyoainishwa katika sura ya Tatu, sehemu ya 81 (i) na (aa).

Alibainisha kuwa upatikanaji dawa na vipimo vya kitabibu kwa uhakika katika kituo cha huduma za afya kwa kiasi kikubwa unaakisi ubora wa huduma zitolewazo na mahali husika.Hivyo, alitoa mwito kwa washiriki kuzingatia utekelezaji wa mwongozo wa mfumo huo ili waweze kuusimamia kikamilifu kwa ajili ya kuleta matokeo chanya yanayolenga kuongeza upatikanaji wa bidhaa za afya kwenye vituo vya kutolea huduma hizo.

Katika hatua nyingine, Mwezeshaji wa kitaifa kutoka Wizara ya TAMISEMI, Emmanuel Mayunga, alisema semina hiyo inalenga kuwajengea uwezo washiriki ili wanapomaliza waweze kusimamia vema Mfumo huo kulingana na mwongozo na sheria za nchi

 Mfamasia Elikana Lubango, alisema mfumo Mshitiri ulianzishwa kwa mujibu washeria za ununuzi wa umma pamoja na mpango mkakati wa kisekta ili kutatua changamoto za upatikanaji wa huduma bora za afya nchini.Alisema Mfumo huo unasaidia wakati bidhaa za afya zinapohitajika kwa dharura kupatikana mara moja tofauti na ilivyokuwa siku za nyuma.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Singida, Victorina Ludovick akizungumza kwenye mafunzo hayo.
Mafunzo yakiendelea.
Wadauwa Sekta ya Afya wakiwa kwenye mafunzo hayo.
 

Share To:

dotto mwaibale

Post A Comment: