Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Dk. Fatuma Mganga, akizungumza  Machi 30, 2023, wakati akifungua kikao cha Umoja wa Walimu Wakuu wa Shule za Sekondari Tanzania (TAHOSSA) Mkoa wa  Singida.

Na Dotto Mwaibale,Singida 

KATIBU Tawala Mkoa wa Singida, Dk. Fatuma Mganga, amesema walimu wana nafasi nzuri ya kuweza kupambana na tatizo la mapenzi ya jinsia moja (ushoga) na usagaji mashuleni kwa kuwa wao ni walezi wa wanafunzi kuanzia ngazi ya chekechea hadi elimu ya juu.

Akizungumza Machi 30, 2023, wakati akifungua kikao cha Umoja wa Walimu Wakuu wa Shule za Sekondari Tanzania (TAHOSSA) Mkoa wa Singida, alisema sasa hivi kumekuwa na tatizo kubwa la ushoga hivyo inatakiwa jitihada za dhati katika kunusuru wanafunzi wasiweze kujiingiza kwenye vitendo hivyo ambavyo ni kinyume na utamaduni wa kitanzania.

Alisema walimu wanaweza kuzuia watoto wasijiingize katika vitendo hivyo kwa kuwa jirani na watoto hao na kufuatilia mienendo yao kwa kushirikiana na wazazi wao.

"Wote tuliona Dk.Harrison Mwakyembe wakati akizungumzia suala la ushoga ambalo walengwa zaidi wanaotafutwa kujiingiza katika vitendo hivyo ni vijana wadogo hivyo walimu chukueni hatua kuwanusuru wanafunzi na janga hilo," alisema.

Akizungumzia taaluma alisema walimu wakiamua wanafunzi wote watafaulu na kuondoa kabisa alama ziro na akawaomba walimu kujenga ushirikiano na wazazi na walezi ili kujua changamoto za watoto wakiwa shuleni na nyumbani jambo litakalosaidia kuwaweka sawa.

Mganga alisema changamoto za watoto darasani haziwezi kuwa za wazazi, mila au desturi bali ni za walimu na akahoji inakuweje watoto asilimia 90 darasani wote wapate alama F.

"Walimu wa enzi zetu wanafunzi walipokuwa wakifanya vibaya katika mitihani yao walikuwa wakiumia sana na ninyi ebu igine hilo kwa ajili ya kuwasaidia watoto" alisema Mganga.

Mganga aliwaomba walimu hao waende wakakomae na hawatashindwa na kupitia wao hakuna litakaloshindikana kwani Serikali inawategemea.

Aliwataka walimu waende kutoa faraja katika familia, waende kutengeneza wasomi, wakafanye kazi kwa uzalendo kwa kuwainua watoto hao kitaaluma na kuwa watapata baraka kutoka kwa wazazi na Mungu.

Mganga alisema Rais Dk. Samia Suluhu Hassan amefanya kazi kubwa ya kujenga miundombinu ya madarasa ili wanafunzi wapate maeneo mazuri ya kusomea ambapo kwa Mkoa wa Singida madarasa 620 yenye thamani ya Sh.Bilioni 12.4 yamejengwa  hivyo njia pekee ya kumuheshimisha ni kufaulisha wanafunzi wote na asiwepo wa kupata daraja la tatu wala ziro bali wapate daraja la kwanza na la pili.

Aidha, Mganga aliwataka walimu hao kuwashirikisha wazazi kukarabati samani za shule zinazo haribika ambazo zimekuwa zikiwekwa katika moja ya madarasa yao badala ya kusubiri Serikali ifanye kazi hiyo.

Akizungumzia suala la chakula kwa wanafunzi aliwataka walimu hao kila shule kuwa na mashamba kwa ajili ya kulima mahindi na mazao mengine na akahimiza suala zima la utunzaji wa mazingira ya shule kwa kupanda miti na maua na wanafunzi wawe na vidumu vya maji kwa ajili ya kumwagilia.

"Kuanzia mwaka ujao tutaanza kufanya mashindano ya utunzaji wa mazingira na shule itakayo shinda tutaipatia zawadi" alisema Mganga.

Mganga pia aliwataka walimu hao kwenda kuanzisha elimu ya kujitegemea katika shule zao kwa kufuga, mbuzi, ng'ombe, kuku na kufungua miradi midogo midogo ambayo itawapatia kipato na kuwajengea uwezo wanafunzi wa kujua mbinu za kujitegemea kuanzia wakiwa shuleni.

Mganga aliwahimiza walimu hao kufanya kazi kwa bidii na kujituma na kuwa adui yake mkubwa ni mtumishi yeyote ambaye atashindwa kufanya hivyo na kuwa  hata mvumilia hata kidogo.

Afisa Elimu Mkoa wa Singida, DK. Elpidius Baganda alisema kazi kubwa wanayotarajia kuifanya ni kupita mashuleni kwa siku sita kila wiki kwa ajili ya kuangalia kama tathmini za mitihani ya kidato cha nne na tatu zilizochukuliwa.

Alisema jambo lingine watakalolitilia kipaumbele ni suala zima la upatikanaji wa chakula mashuleni sambamba na kuangalia miradi mbalimbali ambayo Serikali imetoa fedha nyingi kama imekamilika kwa asilimia 100.

Mwenyekiti wa TAHOSSA, Paskal Kichambati alisema changamoto zao nyingi huwa zinatatuliwa kuanzia ngazi ya wilaya, mkoa hadi taifa na kuwa TAHOSSA kazi yake kubwa ni kuleta utulivu.

Akizungumzia suala la miradi inayofanyika mashuleni chini ya usimamizi wa walimu hao alisema licha ya kuwa ni walimu wamekuwa wahandisi wabobezi kwa kuweza kuisimamia na kukamilika kwa ubora na kwa kiwango cha hali ya juu na kwa thamani ya fedha zilizotolewa na Serikali.

Alisema baadhi ya walimu kwenye akaunti zao za shule  wamekuwa na fedha kuanzia Sh. milioni 30 hadi 80 kwa ajili ya kumalizia miradi hiyo na wamekuwa wazalendo na waaminifu katika matumizi ya fedha hizo.

Mwenyekiti wa TAHOSSA, Paskal Kichambati, akizungumza kwenye kikao hicho. Kulia ni Makamu Mwenyekiti wa TAHOSSA, Method Njiku.
Afisa Elimu Mkoa wa Singida, DK. Elpidius Baganda akizungumzia mikakati waliojiwekea ya utendaji kazi. Kushoto ni Afisa Elimu Taaluma Mkoa wa Singida, Regina Yaghambe.
Walimu wakiwa kwenye kikao hicho.
Kikao kikiendelea.
Taswira ya kikao hicho.
Mwenyekiti wa TAHOSSA Kanda, Mwalimu Jeremia Kitiku akizungumza kwenye kikao hicho.
Walimu wakiwa katika picha ya pamoja na mgeni rasmi wa kikao hicho Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Dk.Fatma Mganga.
Picha ya pamoja.
Mgeni rasmi akiwa katika picha ya pamoja na walimu.
Picha ya pamoja.
Muonekano wa kikao hicho.
Walimu wakifuatilia kila jambo lililokuwa likifanyika kwenye kikao hicho.
Usikivu ukiwa umetawala kwenye kikao hicho.
 

Share To:

dotto mwaibale

Post A Comment: