Na; Elizabeth Paulo,Dodoma

Kutokana na utafiti uliofanywa na Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa kazi kuhusu usajili wa sehemu za kazi pamoja na kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara nchini ilibainika uwepo wa ada ambazo zilikuwa zinaongeza gharama za uendeshaji na kuchangia sehemu nyingi za kazi kutokidhi matakwa ya Sheria na kufifisha ushindani wao kibiashara. 


OSHA ilipendekeza ada hizo kupunguzwa ama kufutwa ambapo Mhe. Rais wa Jamhuriya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan aliridhia ada hizo kufanyiwa marekebisho kwa kuondoa na kupunguza jumla ya Ada / Tozo kumi na tatu 13.


Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa kazi Bi. Khadija Mwenda Amebainisha hayo leo March 3, 2023 Jijini Dodoma wakati wa mkutano na waandishi wa habari alipokua akieleza utekelezaji wa majukumu ya Wakala pamoja na mafanikio Yaliyopatikana katika uongozi wa serikali ya awamu ya Sita.“Ada zilizoolewa ni pamoja na Ada ya Usajili wa eneo la kazi iliyokuwa ikitozwa kati ya Sh. 50,000 hadi Sh.1, 800,000, Ada ya fomu ya usajili sehemu za kazi iliyokuwa ikitozwa Sh. 2,000,Kufuta Faini zinazohusiana na ukosefu wa vifaa vya kuzimia moto ya Sh. 500,000, Kuondoa Ada ya Leseni ya Ithibati iliyokuwa inatozwa Sh 200,000 kwa mwaka, Ada ya Ushauri wa kitaalamu wa Usalama na Afya ya Sh 450,000”.Alisema Bi. Mwenda


Bi. Mwenda Ameendelea kusema Ada zingine Zilizofutwa kuwa ni Ada ya mafunzo ya elimu kwa umma iliyokuwa inatozwa kiasi cha Sh. 250,000 kwa kila mshiriki, Kupunguza ada ya uchunguzi wa ajali iliyokuwa ikitozwa Sh. 500,000 mpaka Sh. 120,000, Kuondoa ada ya Kipimo cha Mzio (Allergy test) iliyokuwa ikitozwa Sh. 25,000 kwa Mfanyakazi.


“Ndugu zangu Ada ya Kipimo cha Kilele cha Upumuaji (Peek Expiratory Flow test) iliyokuwa ikitozwa Sh. 10,000 kwa Mfanyakazi imefutwa , Tumepunguza ada ya huduma za ukaguzi wa mifumo ya umeme katika Vituo vya Mafuta vilivyopo vijijini kutoka Sh. 650,000 hadi Sh. 150,000. Punguzo hili lililenga kuhamasisha uwekezaji katika maeneo hayo, hivyo kupunguza athari zinazoweza kutokea kutokana na utunzaji wa mafuta kwenye chupa za maji na madumu, suala ambalo linahatarisha maisha ya wananchi katika maeneo hayo”AlisemaAda zilizofutwa ama kupunguzwa na OSHA zinatarajiwa kuleta unafuu kwa Wafanyabiashara na Wawekezaji Nchini kwa kuwapunguzia gharama za uendeshaji ambapo kiasi kilicho futwa ama kupunguzwa kinakadiriwa kuwa zaidi ya Shiling Bilioni 35 na kumpendeza Mhe. Rais fedha hizo zitumike katika kuimarisha mifumo ya kulinda wafanyakazi ili waweze kuzalisha kwa tija.


Kwa Mujibu wa Sheria namba 5 ya mwaka 2003 ya Usalama na Afya Mahali pa kazi OSHA imepewa jukumu la Kuishauri Serikali kuhusu masuala ya usalama na afya mahali pa kazi, kuhusiana na Sera, Kanuni na Miongozo mbalimbali ya usimamizi wa usalama na afya nchini ikiwemo kushauri namna ya kuridhia Mikataba ya Kimataifa inayohusu masuala ya usalama na afya.


Pia amesema pamoja na majukumu mengine OSHA wanayojukumu la kuongeza uelewa miongoni mwa wadau yaani kutoa Mafunzo mbalimbali ili kuhakikisha maeneo ya Kazi yanakua na mifumo ya kumlinda mfanyakazi.


Taasisi ya OSHA imepata mafanikio makubwa ambayo yametokana na uongozi wa seriki ya awamu ya Sita yanayoendana na utekelezaji wa Ilani ya Chama Tawala Ibara ya 130 (f) ambapo Chama kimewaahidi Watanzania kwamba kitajenga uwezo wa waajiri na wafanyakazi kuhusu afya na usalama mahali pa kazi.OSHA imefanikiwa kusimika mfumo wa TEHEMA wa Usimamizi wa taarifa za kaguzi nchini (Workplace Inspection Management System (WIMS)) ambapo kupitia mfumo huu, huduma ya utoaji wa taarifa za ukaguzi, ajali na mafunzo unafanyika kwa njia ya kielektroniki


 “Tumepunguza muda wa kupata Cheti cha Usajili wa sehemu za kazi kutoka siku 14 hadi siku 1 kwa kuwa usajili unafanyika kwa njia ya kielektroniki na ambapo mteja ana uwezo kuprinti chake cha usajili popote alipo (Online registration),

Kutoa Leseni ya Kukidhi Matakwa ya Sheria ya Usalama na Afya mahali pa kazi (Compliance License) kutoka siku 28 hadi siku 7 kwa sasa na kupitia mfumo huu waajiri wanaweza kuingiza nyaraka zao zinazohitajika bila kufika katika ofisi za OSHA na kujifanyia tathmini ya namna walivyokidhi viwango vya usalama na afya (Self Assessment) hivyo kurahisha upatikanaji wa leseni na huduma zingine”AlifafanuaMtendaji Mkuu huyo amesema OSHA imeiwezesha Tanzania kupata Dawati la Usalama na Afya mahali pa Kazi katika Nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) na kuw fursa kwa Nchi kuweza kuuza na kubadilishana Utaalamu wa Mifumo ya Uendeshaji wa Taasisi za Usalama na Afya Kimataifa.


Mwakilishi wa Tanzania kutoka OSHA alishindanishwa na wataalamu 48 kutoka katika Nchi 16 za Jumuiya na hatimaye Mwakilishi huyo wa Tanzania, alifanikiwa kuchukua nafasi hiyo ambapo Pamoja na vigezo vingine vilivyotumika kupata mshindi, kigezo kimojawapo kilikuwa ni sifa ya Tanzania kuwa na mfumo madhubuti wa Usalama na Afya mahali pa kazi unaosimamia nguvu kazi na hatimaye kuwezesha kuwepo kwa ajira zenye staha.


“hatua hii ni mafanikio makubwa kwa nchi yetu na OSHA kwa kutambulika Kimataifa kwa kuwa na wataalam wenye uwezo wa kusimamia mifumo ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi kwa kuzingatia vigezo vya Kimataifa.”Katika kusimamia Sheria ya Usalama na Afya kwa lengo la kuzuia ajali, magonjwa na vifo vitokanavyo na kazi, maeneo ya kazi ambayo hayakuzingatia Sheria na Kanuni za Usalama na Afya yalichukuliwa hatua mbali mbali za kisheria zikiwemo kupewa hati ya maboresho (Improvement Notice) ambapo maeneo ya kazi 1,588 yalipewa hati hizo na maeneo ya kazi mengine105 yalitozwa faini. 


Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi ni Wakala wa serikali, chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu- Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu. Wakala huu ulianzishwa mnamo tarehe 31 Agosti, 2001 chini ya Sheria ya Wakala za Serikali Namba 30 ya mwaka 1997 kama sehemu ya maboresho katika utoaji wa Huduma za Serikali kwa Wananchi.


Kusudi la kuanzishwa kwa Wakala huu ilikuwa ni kupata chombo mahsusi cha Serikali chenye jukumu la kuboresha ustawi wa wafanyakazi kwa kusimamia Usalama na Afya mahali pa kazi kupitia Sheria Namba 5 ya Mwaka 2003.Matokeo ya usimamizi huo ni kupunguza ajali, magonjwa na vifo vitokanavyo na kazi Kupitia usimamizi huo kutalinda nguvukazi ya Taifa kwa kuwezesha ajira zenye staha, kulinda mali na mitaji ya wawekezaji ili kuongeza ufanisi na tija katika uzalishaji mali na hatimaye kukuza pato la Taifa.


Ili kutekeleza majukumu yake ipasavyo na kusogeza huduma kwa wananchi Wakala una Ofisi katika Kanda sita 6 katika kuhakikisha Watanzania wanakua salama sehemu za kazi.Share To:

ELIZA DOM

Post A Comment: