Waziri wa Nishati, Mhe. January Makamba akizungumza katika Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Nishati jijini Arusha ambapo pamoja na masuala mengine, Baraza hilo linapitia Mpango wa Bajeti wa Wizara ya Nishati kwa mwaka 2023/2024.


Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato akizungumza katika Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Nishati jijini Arusha ambapo pamoja na masuala mengine, Baraza hilo linapitia Mpango wa Bajeti wa Wizara ya Nishati kwa mwaka 2023/2024.


Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba, akizungumza katika Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Nishati jijini Arusha ambapo pamoja na masuala mengine, Baraza hilo linapitia Mpango wa Bajeti wa Wizara ya Nishati kwa mwaka 2023/2024.


Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Athuman Mbuttuka akifunga Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi Wizara ya Nishati jijini Arusha, tarehe 6 Machi, 2023.


Waziri wa Nishati, Mhe.January Makamba (katikati) na viongozi wengine wa Wizara wakiimba Wimbo wa Wafanyakazi wa Mshikamano kabla ya kufungua Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Nishati jijini Arusha. Wa Tatu kutoka kulia ni Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato, Wa Tatu kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba, Wa Pili kushoto ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Athuman Mbuttuka na wa kwanza kulia ni Katibu wa Baraza la Wafanyakazi Wizara ya Nishati, Fortunata Getele.


Waziri wa Nishati, Mhe.January Makamba (katikati) akiwa katika picha ya pamoja Menejimenti ya Wizara ya Nishati mara baada ya kufungua Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Nishati jijini Arusha. Wa Tatu kutoka kulia ni Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato, Wa Tatu kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba, Wa Pili kushoto ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Athuman Mbuttuka. Wa kwanza kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu, Bahati Mtono, Wengine ni Katibu wa TUGHE Taifa, Meshack Lugeiyamu na Katibu wa Baraza la Wafanyakazi Wizara ya Nishati, Fortunata Getele.


Waziri wa Nishati, Mhe.January Makamba (katikati) akiwa katika picha ya pamoja Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi Wizara ya Nishati, mara baada ya kufungua Mkutano wa Baraza hilo jijini Arusha. Wa Tatu kutoka kulia ni Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato, Wa Tatu kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba, Wa Pili kushoto ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Athuman Mbuttuka. Wa kwanza kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu, Bahati Mtono, Wengine ni Katibu wa TUGHE Taifa, Meshack Lugeiyamu na Katibu wa Baraza la Wafanyakazi Wizara ya Nishati, Fortunata Getele.

*************************

Na Teresia Mhagama

Waziri wa Nishati, Mhe. January Makamba, amesema kuwa, majadiliano yanayohusu Mradi wa Kuchakata na Kusindika Gesi Asilia baina ya Serikali ya Tanzania na wawekezaji Kampuni ya Shell ya Uholanzi na Equinor ya Norway na washirika wao yamekamilika na kwamba sasa wataalam wapo katika kazi ya kuandika mikataba ya mradi huo.

Waziri wa Nishati ameyasema hayo tarehe 06 Machi, 2023 jijini Arusha wakati akitoa vipaumbele vya Wizara katika Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Nishati ambapo pamoja na masuala mengine ya kiutumishi, Baraza hilo limepitia Mpango wa Bajeti wa Wizara ya Nishati kwa mwaka 2023/2024.

“Mazungumzo ya mradi huu wa LNG yamekamilika na wataalam kwa sasa wanaandika mikataba mikubwa miwili yenye masuala mengi ikiwemo ya kiufundi, Mkataba mmoja ni wa Nchi Hodhi (HGA) na mwingine ni mkataba uliounganishwa wa vitalu vya Gesi Asilia Namba I,II na IV ambavyo gesi yake itatumika kwenye mradi wa LNG, kila mkataba una kurasa zaidi ya 600, hii si kazi ndogo ila nimewasisitiza wamalize kazi mwezi huu ili kuweza kuendelea na hatua nyingine za utekelezaji.” Amesema Makamba

Amesema kuwa mradi huo ambao uwekezaji wake ni zaidi ya Shilingi Trilioni 70 utaleta mapinduzi makubwa ya kiuchumi nchini na utaifanya Tanzania kuwa moja ya nchi zinazochangia katika usalama wa nishati duniani hivyo amewataka Watendaji wa Wizara ya Nishati kuendelea kusimamia utekelezaji wa mradi huo.

Makamba ametaja mradi mwingine unaoendelea kutekelezwa ni wa Bomba la Mafuta Ghafi kutoka Uganda hadi Tanzania ambapo kwa sasa shughuli mbalimbali za maandalizi ya ujenzi zinaendelea na mwezi uliopita Serikali imetoa kibali cha ujenzi wa bomba hilo kwa kampuni ya EACOP na kwa sasa inaendelea kukamilisha taratibu za kupata pesa za kutekeleza mradi huo ambazo zimefikia mwishoni.

Ameongeza kuwa, zoezi la ulipaji fidia kwa watu 9800 katika mkuza wa Bomba la mafuta zinaendelea ambapo mpaka sasa shilingi Bilioni 29.2 zimelipwa kati ya shilingi Bilioni 30 zilizokuwa zinahitajika kwenye ulipaji fidia na matarajio ni kwamba ujenzi unatarajiwa kuanza kabla ya mwisho wa mwaka huu.

Ametaja baadhi ya faida zitakazotokana na mradi huo kuwa ni pamoja na ajira 10,000, Serikali kupata mapato kupitia tozo ya kupitisha mafuta, ada mbalimbali kupitia matumizi ya Bandari ya Tanga na kampuni mbalimbali za kitanzania zitatoa huduma katika mradi huo. Pia ujenzi wa bomba unahamasisha shughuli za utafiti na uchimbaji wa mafuta kwani linapita kwenye maeneo yenye viashiria vya upatikanaji wa mafuta hivyo Tanzania ikipata mafuta tayari miundombinu ya usafirishaji mafuta hayo ipo.

Kuhusu hali ya upatikanaji umeme amesema kuwa, kazi ya kurekebisha miundiombinu na kuongeza uzalishaji umeme inaendelea kupitia miradi mbalimbali kama ya gridi imara na hivi karibuni Serikali imesaini mikataba ya takriban ya shilingi Trilioni 1.9 ya kurekebisha miundombinu ya umeme. Amesema kuwa, kazi hiyo inachukua muda hivyo amewaomba watanzania wawe na subira ili matunda ya uwekezaji kama huo yaonekane.

Kuhusu Nishati Safi ya Kupikia, amesema kuwa hiyo ni ajenda ya Wizara ya Nishati kwani ni suala linalowagusa watanzania wote kuanzia mtu maskini hadi tajiri hivyo Serikali ambayo ina jukumu la kuboresha maisha ya watanzania inalisimamia suala hilo ili nchi iingie kwenye nishati safi ya kupikia huku akitolea mfano nchi ya India ambayo asilimia 98 ya wananchi wake hawatumii kuni na mkaa .

“Kamati inayohusika na mradi huu wa Nishati Safi ya Kupikia inafanya kazi na kabla ya Bajeti ya Mwaka 2023/2024, Serikali itatoa Dira, Mkakati na Mwelekeo wa kuondokana na matumizi ya nishati chafu na isiyo salama kwa takriban asilimia 80 ndani ya miaka 10, na haya ni maelekezo ya Mhe,Rais hivyo lazima tuyatekeleze.” Ameeleza Makamba

Katika hatua nyingine, Makamba amewataka watendaji wa Wizara kubuni vyanzo vya mapato vya kutekeleza miradi ya Nishati na kutoitegemea Serikali pekee hivyo amewaelekeza watendaji hao kushirikisha sekta binafsi ili kutekeleza miradi ya nishati.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato alimshukuru Waziri wa Nishati kwa ubunifu wa miradi mbalimbali itakayoboresha Sekta ya Nishati nchini na kwamba chini ya uongozi wake tayari kuna mafanikio yanaonekana na kuahidi kuwa watendaji wa Wizara wataendelea kufanya kazi kwa ari mpya, kasi mpya na nguvu mpya.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba alimshukuru Waziri kwa jitihada mbalimbali na msukumo anaoutoa katika Sekta ya Nishati nchini ikiwemo suala la uwepo wa Nishati Safi ya Kupikia na kusema kuwa Watumishi na viongozi wa Wizara watafanya kila jitihadi ili kutekeleza miongozo anayoitoa.

Akifunga Mkutano huo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Athuman Mbuttuka amesema kuwa masuala yote yaliyoelekezwa na Viongozi Wakuu wa Wizara yatafanyiwa kazi na kwamba kuna kazi kubwa ya kutekeleza masuala hayo, pia amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kumteua kuhudumu katika Sekta ya Nishati na pia amesisitiza uwepo wa ushirikiano katika kutekeleza masuala mbalimbali ya Wizara.

Share To:

emmanuel mbatilo

Post A Comment: