Na; Elizabeth Paulo, Dodoma 


Jeshi la ulinzi la wananchi wa Tanzania limetangaza nafasi za kujiunga na Jeshi kwa vijana wa kitanzania wenye elimu ya kuanzia kidato cha nne hadi Shahada ya Uzamili.


Nafasi hizo ni kwa wale waliomaliza mkataba wa mafunzo ya kujitolea kutumikia Jeshi la kujenga Taifa (JKT).


Kaimu Mkurugenzi wa Habari na Uhusiano Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Luteni Kanali Gaudentius Gervas Ilonda ametoa taarifa ya nafasi za kujiunga na Jeshi hilo wakati wa mkutano na waandishi wa habari leo Machi 09, 2023 kwenye ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO) jijini Dodoma.


"Mwombaji anatakiwa awe raia wa Tanzania wa kuzaliwa mwenye Kitambulisho cha Taifa, awe na umri wa miaka 18 hadi 26 kwa wenye elimu ya kidato cha nne hadi kidato cha sita na umri usiozidi miaka 27 kwa wenye elimu ya juu". Alisema Ilonda



Amesema mwombaji anatakiwa kuwa na afya nzuri na akili timamu, awe Mtanzania mwenye tabia na nidhamu nzuri ambaye hajapatikana na hatia ya makosa ya jinai Mahakamani na kufungwa pia asiwe ameoa au kuolewa.


"Awe na cheti halisi cha kuzaliwa, vyeti vya shule na vyeti vya Taaluma, awe hajatumikia Jeshi la Polisi, Magereza, Chuo cha Mafunzo au Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo pia awe amehitimu mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa kwa Mkataba wa kujitolea miaka miwill (2) na kutunukiwa cheti".Alisema  


Na kuongeza"Maombi yote yaandikwe kwa mkono na yawasilishwe Makao Makuu ya Jeshi Dodoma kuanzia tarehe ya tangazo hili hadi tarehe 20 Machi, 2023 yakiwa na viambatisho ikiwemo nakala ya Kitambulisho cha Taifa au namba ya NIDA".Alifafanua


Kadhalika amesema Viambatisho vingine ni nakala ya cheti cha kuzaliwa, vyeti vya shule na chuo, nakala ya cheti cha JKT pamoja na namba ya simu ya mkononi ya mwombaji.


"Maombi hayo yatumwe kupitia anuani ya;

Mkuu wa Utumishi,

Makao Makuu ya Jeshi,

Sanduku la Posta 194,DODOMA, Tanzania au katika barua pepe ya ulinzimagazine@tpdf.mil.tz".Alieleza



Pia Luteni Kanali Ilonda amewataka wananchi kuwa makini na matapeli kwani kumekuwa na tabia ya kuibuka matapeli pindi matangazo hayo ya nafasi ya kujiunga na jeshi hili zinapotangazwa


"Natambua katika matangazo haya ya kujiunga na nafasi hizi kuna matapeli watajitokeza na kuanza kupenyeza utapeli wao ,hivyo watanzania wasidanganyike wala kurubuniwa na hakuna njia ya mkato katika kupata nafasi hizi zaidi ya kuzingatia vigezo vilicyowekwa wazi kabisa,


"Matapeli ni Binadamu hivyo kutokana na kukua kwa teknolojia kila siku wanabuni mbinu mpya hivyo inabidi kuchukua tahadhari kwa pamoja ili kuepukana na mitego ya utapeli wao,"Amesema Luteni Kanali Ilonda




Kwa mujibu wa Luteni Kanali Ilonda Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania hakuna ajira bali kuandikishwa.


"yeyote mnayemuona katika jeshi hili ameandikishwa kwa kulitumikia Taifa, hivyo hakuna mshahara ila kuna posho, JKT hatuingizi mtu kama anakwenda kuajiriwa, badala yake anaenda kupata stadi za maisha na uzalendo wa kulinda taifa lake.



Share To:

ELIZA DOM

Post A Comment: