JENGO la kuhifadhia vifaa tiba na dawa zilizoisha muda wake mkabala na hospitali teule ya rufaa ya Mkoa wa Geita Mtaa wa Nyanza mjini Geita limetekea kwa moto huku chanzo chake hakijafahamika.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Berthaneema Mlay amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kueleza tukio hilo lilitokea leo Machi 27, 2023 majira ya saa saba mchana.

Amesema baada ya kupata taarifa za ajali, jeshi la polisi na jeshi la zimamoto na uokoaji walifika eneo la tukio kwa wakati na kujitahidi kuzima moto ambao uliendelea kutokana na madawa yaliyokuwepo.

“Tuliweza kuwasiliana na wadau wetu ambao ni GGML, ambao walifika kwa haraka, na kufanikiwa kuzima moto huo. Hakuna madhara kwa binadamu bali ni jengo pekee ndio limeungua.

“Lakini pia bado tathimini au thamani ya vitu vilivyoungua bado haijajulikana, tusubiri wahusika wakifanya tathimini tutaweza kujua ni vitu vya thamani gani vimeungua,” amesema.

Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoani Geita, Edward Lukuba amesema walipata taarifa hizo majira ya saa saba mcahana na kuwahi eneo la tukio ili kupunguza athari za moto.

“Tulikuta moto ushakuwa mkubwa, lakini tulifanikiwa kuupunguza makali huo moto, na kuweza kudhibiti hali ya moto huo usiweze kusambaa maeneo mengine.

“Hili jengo lililoshika moto, ni jengo linalomilikiwa na Halmashauri ya mji wa Geita, lakini limekuwa likitumika kama ghala la kuhifadhia vifaa tiba na madawa vilivyoisha muda wake,” amesema.

Share To:

Post A Comment: