Na John Walter-Manyara


Wanaume wametakiwa kuacha kukaa kimya pindi wanapofanyiwa vitendo vya ukatili na wake zao.

Wito huo umetolewa na Mkaguzi msaidizi wa jeshi la polisi Witnes Kimario, mkuu wa dawati la Junsia Polisi mkoa wa Manyara , wakati wa maadhimisho ya siku ya wanawake duniani ambapo katika mji wa Babati yameadhimishwa leo Machi 13, 2023 katika uwanja wa Kwaraa baada ya siku husika machi 8,2023 kuwepo kwa shughuli nyingine iliyolazimu kusogezwa mbele.  

“Tunawaomba wakina baba wasiogope kwa sababu na wao ni sehemu ya wahanga wa ukatili wa kijinsia” alisema Kimario

Amesema wanaume watakapotoa taarifa, zitapatikana takwimu sahihi za matukio ya ukatili wa kijinsia.

Aidha mkuu huyo wa dawati la jinsia polisi mkoa wa Manyara, ametoa wito kwa wakina mama kuendelea kuwa wanaharakati wa kupinga ukatili wa kijinsia kwa kuripoti Polisi vitendo hivyo ili hatua zichukuliwe kwa wahusika.

Aidha ameitaka jamii kutoa taarifa hata kama wataona kiashiria cha ukatili na sio kusubiri hadi utekelezwe.

Kimario amesisitiza kuwa baada ya kutoa taarifa kuhusu vitendo hivyo ni muhimu kufika pia mahakamani kutoa ushahidi kama ili kuithibitishia mahakama na hatua ziweze kuchukuliwa kwa mhusika.

Amesema kwenye jamii kuna baadhi ya wanawake wanafanya vitendo vya kikatili ikiwemo kuwapiga waume zao na kutelekeza watoto.

“Tuendelee kuzikomboa na kuzipigania familia zetu kwa kupinga unywaji wa pombe uliopitiliza, kwa kupinga Imani za kishirikina, kwa kuzikataa na kuzikemea mila na desturi potofu ambazo zimekuwa ndio vyanzo vya kwenye ukatili wa kijinsia”

Amesema kesi za ukatili wa kijinsia hazipaswi kumalizwa kinyumbani na badala yake kesi hizo ziripotiwe kwenye vyombo vinavyohusika ili kutokomeza vitendo hivyo.

Takwimu zinaonesha kuwa mkoa wa Manyara umeshika nafasi ya kwanza kitaifa kwa vitendo vya kikatili na nafasi ya kwanza kwa vitendo vya ukeketetaji.

Kwa mwaka jana vitendo vya ukatili mkoa wa Manyara ulishika nafasi ya pili.

Mkuu wa mkoa wa Manyara Charles Makongoro Nyerere anasema takwimu hizo zinautia dosari mkoa.

Nyerere amewataka wananchi kushirikiana na serikali na wadau wengine kupinga vitendo vya kikatili vilivyoshamiri katika mkoa huo.

Katibu tawala mkoa wa Manyara Carolina Mthapula amewataka wazazi watimize wajibu wao wa kufanya malezi bora kwa watoto wao pamoja na walimu shuleni.

Share To:

Post A Comment: