Mkuu wa wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro Mhe.Kasilda Mgeni amemtaka mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri hiyo Anastazia Tutuba kushirikisha vyombo vya usalama kujua walipo wanafunzi ambao walipashwa kuanza kidato cha kwanza mwaka huu 2023 lakini bado hawajaripoti katika shule walizo pangiwa.


Ameyasema hayo muda mfupi baada ya kufanyika makabidhiano ya Ofisi baina yake na Aliyekua mkuu wa wilaya hiyo Edward Mpogoro ambae amehamishiwa wilaya ya ilala katika uteuzi wa hivi karibuni uliofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan.


“Nimepata taarifa ofisi ya Mkurugenzi kwamba mpaka sasa wanafunzi wa kidato cha kwanza waliokwisha ripoti ni asilimia 89 tu, sioni sababu kwanini iwe asilimia hiyo ninachotaka ni kuona wanafunzi wote waliochaguliwa wanaenda kuripoti katika shule walizopangiwa vinginevyo chukueni hatua”.Alisema Mkuu huyo wa wilaya.


Mbali na msisitizo huo kutaka ufuatiliaji, amewataka viongozi wengine wakiwemo Madiwani, kuendelea kutoa elimu na kuwa mstari wa mbele kukemea matukio ya ukiukwaji wa haki za watoto ikiwa ni pamoja na kuwafichua watu wenye mchezo mchafu kuanzisha mahusiano ya kimapenzi na watoto wadogo wakiwemo wanafunzi.


“Miongoni mwa mambo ambayo nitakua mkali na sitamuonea mtu huruma ni kwenye mambo ya ukatili, sitaki tufike mbali najua hapa kuna viongozi wa kila ngazi tushirikiane kutoa elimu na kukemea kuanzia ngazi za familia ili yasitokee”.Alisema mkuu huyo wa wilaya.



Awali katika makabidhiano hayo aliyekua mkuu wa wilaya hiyo Edward Mpogoro (Mkuu wa wilaya ya Ilala kwa sasa) amewataka viongozi wa wilaya hiyo kuendeleza ushirikiano uliodumu kwa kipindi chote cha uongozi wake na kwamba suala hilo la usimamizi wa elimu ni mwendelezo wa kazi iliyokwisha anza.

Share To:

mwangaza wa hbari

Post A Comment: