Na FARIDA MANGUBE 

Uongozi wa wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro umeiomba serikali kuu kutazama kwa karibu Mradi mkubwa wa Maji Same-Mwanga-Korogwe, uliopangwa kugharimu zaidi ya shilingi Bilioni 600 utakapokamilika, mradi wa muda mrefu ulioanza tangu mwaka 2014.

Mradi huo ni miongoni mwa miradi mikubwa inayotekelezwa na Serikali kwa lengo la kuondoa Kero ya Maji kwa wakazi wa Miji ya Same na Mwanga pamoja na vijiji 38 vilivyo katika eneo la Mradi, ukitazamiwa kunufaisha wananchi wapatao 438,931 katika wilaya za Same (246,793) Mwanga (177,085) mkoani Kilimanjaro na Korogwe 15,053 katika mkoa wa Tanga.

Gharama za utekelezaji wa Mradi huo zinakadiliwa kufikia Dola za Marekani Milioni 300 ambazo ni sawa na Shilingi za Tanzania Bilioni 669.

Mkuu wa wilaya ya Same Mhe.Kasilda Mgeni wakati alipotembelea Mradi huo, alisema kutokana na maelezo wa wasimamizi kuna haja ya kupeleka ombi maalum kwa viongozi wa serikali kuu kuomba nguvu zaidi katika msukumo wa upatikanaji wa fedha ili mradi huo uweze kukamilika na kuwanufaisha wanachi. 

“Ninaimani na viongozi wangu, kila siku tunamuaona Waziri wa Maji akihangaika na Miradi ya Maji naamini kabisa chini ya Rais wetu kipenzi Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassani Mradi huu utakamilika”.Alisema Mkuu huyo wa Wilaya ya Same.

Kwa upande wake msimamizi wa Mradi huo kutoka kampuni ya Don Consult Ltd. Mhandisi Fredrick Chuwa alisema mradi huo umepangwa kutekelezwa kwa awamu mbili, awamu ya kwanza ni ujenzi wa Miundombinu ya Uzalishaji  wa Maji Safi,salamana ya uhakika pamoja na usambazaji wa Maji katika Mji wa Same,Mwanga na Vijiji 9 na awamu ya Pili ni usambazaji wa Maji katika Vijiji 29 vilivyo katika eneo la Mradi.

“Ujenzi ukikamilika Mradi utakua na uwezo wa kuzalisha Maji Lita Milioni 87.099 kwa siku ikilinganishwa na mahitaji ya sasa ambayo ni Lita Milioni 78.38 kwa siku”.Alisema Mhandisi Chua.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Same Mwanga Mhandisi Christopher Kiwone, Mahitaji ya Maji kwa Mji wa Same ni wastani wa Mita za Ujazo 3,926 kwa siku lakini kiwango halisi cha utoaji wa huduma ya maji safi na salama ni wastani wa Mita za Ujazo 1,845 sawa na asilimia 47.

“Changamoto za hapa ni pamoja na Uchakavu wa miundombinu iliyopo sasa hasa Bomba unaosababisha upotevu wa Maji,Ufinyu wa Mtandao w miundombinu ya usambazaji, Uzalishaji mdogo ikilinganisha na mahitaji hivyo Utekelezaji wa Mradi mkubwa wa Same-Mwanga-Korogwe huduma ya Maji itaboreka na kufikia asilimia 100 utakapo kamilika ambapo hadi kufikia Disemba mwaka 2022 utekelezaji wa Mradi huo katika mji wa Same ulikua asilimia 88”.Alisema Mhandisi Mkurugenzi wa wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa mazingira Same-Mwanga Eng.Christopher Kiwone.
Share To:

mwangaza wa hbari

Post A Comment: