NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

Waziri ardhi nyumba na maendeleo ya makazi Dkt. Angelina Mabula ametoa wito kwa taasisi za umma na binafsi pamoja na watu binafsi kulipa kodi ya ardhi pamoja na madeni wanayodaiwa katika kipindi hiki cha miezi mitatu ya msamaha wa riba kabla hatua kali za kisheria hazijachukuliwa ikiwemo kunyang'anywa maeneo yao.

Dkt. Mabula ametoa wito huo Jana Februari 14,2023 katika Mkutano wa Pili wa Majadiliano ya Kisekta kati ya Wizara hiyo na Wadau wa Sekta ya Ardhi ambapo amesema kuanzia Februari hadi Aprili Mwaka huu Serikali imeongeza muda wa msamaha wa riba ili kuwapa unafuu wale walioshindwa kulipa madeni yao kutokana na malimbikizo ya madeni hayo.

Amesema mwaka wa huu wa fedha serikali imepata mkopo wa fedha kutoka Benki ya Dunia shilingi bilioni 345 kwa ajili ya utekelezaji mradi wa uboreshaji usalama wa miliki za ardhi itakayorahisisha upimaji wa maeneo na kutatua migogoro.

Aidha amesema, kupitia mkutano huo wa awali, Wizara imeyafanyia kazi maoni na hoja za wachangiaji 53 kwenye maeneo makubwa 15, na kufuatia hoja na maoni hayo, Waziri Dkt.Mabula amesema, Wizara imeandaa Bangokitita linalotoa ufafanuzi wa kina kuhusu walivyoshughulikia maoni, hoja na mapendekezo yaliyotolewa.

"Naomba nitoe mrejesho kwa ufupi wa baadhi ya maoni, hoja na mapendekezo muhimu yaliyofanyiwa kazi hadi sasa, kwanza, madeni na malimbikizo makubwa ya kodi ya pango la ardhi kwa wamiliki wa vipande vya ardhi nchini". Amesema

Baadhi ya washiriki katika mkutano huo wameeleza manufaa yatakayopatikana katika mradi uboreshaji usalama wa miliki za ardhi ambayo ni pamoja na upelekaji wa huduma jamii kutokana maeneo hayo kutambulika baada ya kupimwa.
Share To:

emmanuel mbatilo

Post A Comment: