IMG-20230220-WA0093

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Angellah Kairuki amepiga marufuku tabia ya baadhi ya watendaji wa Serikali kuwa na kampuni binafsi za ujenzi,kwani kufanya hivyo ni kinyume na maadili ya utumishi wa umma ambapo imekuwa ikisababisha mgongano wa kimaslahi.

Marufuku hiyo ameitoa leo Februari 20 wakati akizungumza katika Mkutano wa siku moja wa Wahandisi wa Sekretarieti za mikoa,mameneja wa mikoa na wilaya wa TARURA na Wakuu wa Idara za miundombinu na maendeleo vijijini na mijini kwenye mamlaka za serikali za mitaa , uliyofanyika katika ukumbi wa Jiji la Dodoma ,Mtumba.

"Mtu huwezi kujichukulia hatua mwenyewe hivyo kwa yeyote mwenye kampuni binafsi ya ujenzi ajichunguze itamletea mgogoro mkubwa na sisi kama Serikali hatuwezi kumvumilia Mtumishi wetu ambaye anakiuka kwa makusudi sheria ya maadili ya utumishi wa umma,"

Na kuongeza kuwa "kuwa na kampuni binafsi inasababisha mgongano wa kimaslahi hivyo ni ngumu sana kufanya kazi kwa ufanisi na kuzingatia mkataba kwani wewe ndio kila kitu hilo halivumiliki na unakwamisha malengo ya serikali kuwafikishia wananchi maendeleo,"amesema Mhe.Kairuki

Pia Waziri huyo amewataka watumishi hao kuhakikisha wanatimiza wajibu wao kwa ufanisi hasa kusimamia fedha zote zinazopelekwa katika halmashauri zitumike kwa wakati na kuzingatia thamani ya fedha ili kuweza kufikia malengo yaliyokusudiwa.

"Hakuna watumishi wengine wanayoweza kufanya haya zaidi yenu nyinyi katika maeneo yenu ndio maana bajeti ya uratibu na ufuatiliaji imeongezeka nitashangaa msipokwenda kukagua miradi ,tambueni wajibu mkubwa mlionao wa kuhakikisha wahandisi wanazingatia mikataba yao ikiwemo kufanya kazi kwa wakati na kuzingatia thamani ya mradi,"amesisitiza Mhe.Kairuki

Mhe.Kairuki amewaagiza TARURA kuwakata gharama wakandarasi wanaochelewesha ukamilishwaji wa miradi na wanaokwenda kinyume na mikataba pasipo na sababu za msingi kwani wanachelewesha huduma iliyokusudiwa kwa wananchi.

Aidha ,Mhe.Kairuki amebainisha kuwa tangu kuanzishwa kwa TARURA mwaka 2017 kumekuwa na ongezeko la barabara zilizojengwa kwa kiwango cha lami kwa asilimia 96 na barabara zilizojengwa kwa kiwango cha changarawe kwa asilimia 45.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe.David Silinde amesema kuwa TARURA imekuwa ikifanya kazi nzuri ila changamoto yao hawatangazi ili wanachi waweze kufahamu miradi hiyo mikubwa inayotekezwa na Serikali kupitia wakala huyo.

"Mbali na kutangaza mambo makubwa mnayoyafanya toeni taarifa sahihi na hakikisheni ahadi zinazotolewa na viongozi katika ziara mbalimbali zinatekelezwa maana wananchi wanatamani kusikia na kuona ahadi zinazotolewa zinatekelezwa ,msije kufanya viongozi waonekane kuwa na ahadi za uongo kwa wananchi wao,"amesema Silinde.

Naye Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Mhandisi Victor Seff, amesema kuwa mpaka sasa wamefanyia kazi ya ukarabati wa miundombinu ya mtandao wa barabara wenye kilometa 144,419 katika mikoa na halmashauri hapa nchini.

Mhandisi Seff amegusia hali ya mtandao wa barabara ,ambapo amesema mtandao wa barabara wenye urefu wa kilometa elfu 38,868 zina hali nzuri,kilometa elfu 48,307 zipo katika hali ya wastani na kilometa elfu 57,000 ipo katika hali mbaya.
Share To:

emmanuel mbatilo

Post A Comment: