BARAZA la madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Chato mkoani Geita, limesikitishwa na tabia za mtendaji wa kijiji cha Nyarutefye kata ya Buziku kuingia ofisini akiwa na panga kwa lengo la kujihami.


Kitendo hicho ambacho kwa mujibu wa sheria za Tanzania ni kosa la jinai,linatajwa kuwa utaratibu wa kawaida kwa mtendaji huyo kuingia kazini na kutoka akiwa na silaha hiyo baridi.

Diwani wa kata ya Buziku, Salama Mgassa,amelieleza baraza la madiwani wa halmashauri hiyo leo wakati akiwasilisha taarifa za maendeleo ya kata yake,huku akiomba kubadilishiwa mtumishi huyo kutokana na vitendo vinavyotishia amani kwa wananchi.

"Mwenyekiti niliombe Baraza lako lisaidie kupata mtendaji mwingine kutokana na aliyepo kwenye kijiji cha Nyarutefye kuingia ofsini kwake akiwa na panga ambalo hudai ni kwaajili ya kujihami" amesema Mgassa. 

Kauli hiyo mbali na kuibua mshituko mkubwa kwa madiwani hao,wamesema ipo haja kubwa kwa serikali kumuondoa mtendaji huyo kwenye kituo hicho na kupangiwa sehemu nyingine wakati mwajili wake akiwa anatafuta namna ya kumwajibisha.

Share To:

Post A Comment: