Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango ametoa wito kwa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu kuzingatia Mamlaka yake ili kuepukana  na  malalamiko ya nchi wanachama ya kuingilia uhuru wa ndani wa nchi hali inayopelekea baadhi ya Nchi Wanachama kuondoa matamko ya kujiweka chini ya mamlaka ya Mahakama hiyo huku baadhi zikisita kuridhia Mkataba ulioanzisha Mahakama hiyo.

Makamu wa Rais amesema hayo leo tarehe 20 Februari 2023, wakati wa Ufunguzi wa Mwaka wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na watu, uliofanyika Makao Makuu ya Mahakama hiyo Mkoani Arusha. Amesema changamoto zinazopaswa kufanyiwa kazi ni pamoja na zile za kusikiliza na kutolea hukumu mashauri ambayo yako nje ya mamlaka ya mahakama hiyo, Mahakama kutoa  hukumu dhidi ya nchi wanachama bila kuzingatia mazingira na mifumo ya kisheria ya nchi za Afrika na kupelekea hukumu hizo kutotekelezeka. Ameongeza kwamba njia ya mazungumzo kati ya Mahakama na Nchi Wanachama inapaswa kutumika ili malengo yaliyokusudiwa ya Mahakama hiyo yaweze kufikiwa.

Makamu wa Rais amempongeza Rais wa Mahakama hiyo Mheshimiwa Jaji Imani Aboud, kwa hatua anazochukua kuimarisha mahusiano kati ya Mahakama hiyo na Nchi Wanachama na kumsihi kuendeleza jitihada hizo.

Makamu wa Rais amesema Tanzania ina dhamira ya dhati kutekeleza malengo ya Umoja wa Afrika na utekelezaji wa Ajenda 2063 pamoja na kushiriki katika kujenga Taasisi imara za Afrika ikiwa ni pamoja na Mahakama ya Afrika. Amesema kwa kutambua wajibu wa kuhamasisha na kutetea  haki za binadamu, Tanzania imeendelea kuwa chini ya mamlaka ya Mahakama ya Haki  ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu pamoja na  kusaini  na kuridhia mikataba mbalimbali ya kimataifa ya haki za

binadamu.

 

Halikdhalika Makamu wa Rais Dkt. Mpango ametoa wito kwa Mahakama za ndani kuongeza matumizi ya sheria na maamuzi ya mahakama za kimataifa kwa kuongeza matumizi ya TEHAMA ili kuwezesha majaji na wanasheria kupata sheria na maamuzi ya mahakama za kimataifa kwa urahisi. Pia Makamu wa Rais ameiasa Mahakama ya Afrika kuendelea kufanya makongamano ya sheria yatakayokutanisha wadau mbalimbali wa sheria kutoka nchi zenye mifumo tofauti ya sheria ili kuwezesha katika kujifunza na kubadilishana uzoefu.

Vilevile Makamu wa Rais ametoa wito kwa vyombo vya utoaji haki vya ndani ya nchi kujifunza pamoja na kutumia sheria na maamuzi  ya mahakama za haki za binadamu za kikanda na kimataifa ili kufikia maamuzi katika masuala ya haki za binadamu kwa kuzingatia sheria, hukumu na mazingira ya ndani ya nchi husika katika kufikia uamuzi hayo.

Makamu wa Rais ameipongeza Mahakama hiyo kwa mafanikio makubwa iliyofikia katika kulinda na kutetea haki za binadamu tangu ilipoanzishwa. Ameyataja mafanikio hayo ni pamoja na kusikiliza na kutoa hukumu mbalimbali zinazolinda na kutetea haki za binadamu, kuendeleza mjadala na wadau na nchi wanachama wa umoja wa Afrika kuhusu haki za binadamu na kutoa elimu ya haki za binadamu kwa wadau mbalimbali.

 

Kwa upande wake Rais wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu Mheshimiwa Jaji Imani Aboud amesema ni vigumu kwa  malengo ya Umoja wa Afrika ya Ajenda 2063 kufikiwa bila kuwepo msingi imara wa haki za binadamu kwani ustawi, umoja, utangamano, maendeleo, ulinzi na usalama pamoja na utangamano katika jumuiya za kimataifa unafungamanishwa na  haki za binadamu.

Amesema Mahakama huru ni chanzo cha maendeleo ya kijamii na kiuchumi pamoja na kisiasa kwa jamii yeyote ile. Ameongeza kwamba tangu kuanzishwa kwa Mahakama hiyo tayari imetoa hukumu zaidi ya mia mbili ambazo zinagusa nyanja mbalimbali za maisha ya kila siku ya wananchi.

Share To:

Post A Comment: