Na John Walter-Babati.

Wananchi wa kata ya Ayalagaya Halmashauri ya wilaya ya Babati mkoani Manyara wamesema hawapo tayari kusimamiwa na mamlaka ya maji safi na Usafi wa Mazingira (BAWASA) na badala yake wanawataka wakala wa maji vijijini (RUWASA).

Hayo yameelezwa Februari 23,2023 na Diwani wa kata hiyo mheshimiwa Sabini John wakati akiwasilisha kwa mkuu wa wilaya ya Babati Lazaro Twange juu ya ombi la wananchi kutumia wakala wa maji vijijini RUWASA na si BAWASA.

Wananchi hao wameeleza sababu za ombi hilo kuwa ni kutokana na bili kubwa za maji zinazotolewa na BAWASA huku BAWASA wakidai bili kubwa zinatokana na gharama kubwa za uendeshaji.

"Sisi kata ya Alagaya Changamoto tuliyonayo ni maji ambapo jamii ya kata ya Ayalagaya katika mzunguko wangu wa ziara wamependekeza wasimamiwe na RUWASA badala ya BAWASA" alisema Sabini

Amesema wameshaandika barua na kutuma kwa Waziri wa maji kupitia mbunge wao na kwamba waziri aliahidi kufika katika kata ya Ayalagaya lakini hadi sasa hawajamuona.

Baada ya kikao hicho Diwani Sabini amewaambia waandishi wa habari kuwa "Tunamshukuru sana mkuu wetu wa wilaya ya Babati tumeshirikiana naye katika kikao cha WODC, kuna mambo tumempa ushauri naye amepokea kuhusu jambo hili la maji, ataenda kukaa na viongozi wenzake na sisi yale mambo aliyotuelekeza tutatekeleza kama tulivyokubaliana"  

Nje ya kikao hicho, Mkuu wa Wilaya ya Babati Lazaro Twange baada ya kuzungumza na kamati ya maendeleo ya kata (WODC) na viongozi wa chama cha Mapinduzi,  amesema wamekubaliana kwa pamoja kumaliza kinachoendelea na muda wowote watatoa mrejesho wa suala hilo.

Aidha Twange amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za miradi mikubwa ya maji ambayo inatekelezwa kwa kasi wilayani humo na kuahidi kuendelea kusimamia rasilimali hiyo muhimu kwa binadamu na viumbe hai ili kuwafikia ambao bado hawajafikiwa.

Kwa upande wake mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi kata ya Ayalagaya Selestin Silaa amesema wanachotaka wao ni amani ili shughuli za maendelo ziendelee, hivyo wanasubiri mrejesho wa majadiliano waliyoyafanya na mkuu wa wilaya.

 

Share To:

Post A Comment: