IMG-20230224-WA0178

Na. Majid Abdulkarim, Mpimbwe–Katavi

Serikali kupitia Wizara ya Afya imeelekeza wazazi na walezi Mkoani Katavi kupeleka watoto wote wenye umri chini ya miaka mitano kupata chanjo ya kujikinga na ugonjwa wa surua.

Agizo hilo limetolewa na Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu leo akiwa katika ziara ya kikazi ya kukagua hali ya utoaji wa huduma za afya na kuzindua kampeni ya kuongeza kasi na hamasa ya chanjo ya Surua kwa Halmashauri ya Mpimbwe Wilayani Mlele mkoa wa Katavi.

Amesema kuwa anayo mamlaka ya kisheria chini ya Sheria ya Afya ya Jamii kuamua chanjo za watoto za kuwakinga na Surua si hiari ni lazima, hivyo amewataka Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa kuwachukulia hatua wazazi na walezi wote ambao watashindwa kuhakikisha watoto wao wanapata chanjo ya Surua.

“Hatuwezi kukubali kama Serikali kuona watoto wanapoteza maisha wakati tuna uwezo wa kuwakinga kwa kuwapatia chanjo ya surua mapema” amesisitiza Mhe.Ummy.

IMG-20230224-WA0180

Mhe. Ummy amebainisha kuwa kuna watoto zaidi ya 400,000 nchini ambao hawajapata chanjo ya ugonjwa wa Surua na vifo vilivyoripotiwa hadi sasa ni vifo 13 kati ya hivyo vifo 11 vimetokea kwenye jamii, vifo 2 hospitalini na hivyo ni kutokana na wagonjwa kuchelewa kufika katika vituo vya kutolea huduma za afya.

“Kwa hiyo leo tupo hapa Majimoto Mpimbwe kuwaunga mkono wana Mpimbwe na wana Majimoto ili tuishinde Surua lazima watoto wote chini ya umri wa miaka mitano wakamilishe dozi ya chanjo ya surua”, amesema Mhe. Ummy 

Hata hivyo ameongeza kuwa kila watoto 100 wenye Surua katika Halmashauri ya Mpimbwe, watoto 40 wanatoka kata ya Maji Moto.

IMG-20230224-WA0186

Pia katika ziara yake Mhe. Ummy amezindua msafara wa bodaboda/pikipiki na magari kumi ya kutoa elimu na hamasa ya chanjo kwa wananchi wa Mpimbwe ili kupata uelewa wa kupeleka watoto kupata chanjo ya surua mapema.

Pia amesema magari mengine matano yatapelekwa Halmashauri ya Mlele na magari matano yatapelekwa Halmashauri ya Tanganyika.

Ameeleza kuwa watafanya zoezi la nyumba kwa nyumba kuhakikisha kila mtoto mwenye umri wa chini ya miaka mitano anapata chanjo hivyo wasioneane aibu kwa magonjwa yanayowapoteza watoto.

IMG-20230224-WA0176

Mhe. Ummy ameeleza kuwa Surua inaweza kukingwa kwa kutumia chanjo, lakini hata mtoto aliyepata chanjo akipata Surua haitakuwa kali tofauti na yule ambaye hakupata kabisa vilevile na Uviko-19 ndio maana hatuna mgonjwa hata mmoja ICU kwa sasa.

Vile vile ameongeza kuwa kinga ni bora kuliko tiba hivyo ametoa wito kwa viongozi wa dini kutumia nyumba za ibada kuwahimiza waumini wao kuwapeleka watoto kupata chanjo ya Surua ya chanjo. 

Waziri Ummy amesema hata vitabu vitakatifu vya dini vinazungumzia jinsi mwanadamu alivyopewa akili, maarifa na maono hivyo hata chanjo ya Surua ni maarifa katika kujikinga na maradhi hayo.

IMG-20230224-WA0185

Aidha Waziri Ummy amewataka Waganga wa Tiba Asili nao kuhimiza chanjo ya Surua na pia kuhimiza wateja wao wenye dalili za ugonjwa wa huo kwenda kwenye Vituo vya kutoa huduma za Afya

Lakini pia amewataka Maafisa afya wote wa halmashari nchini kupita katika maeneo yote na yanayotoa huduma za kijamii kuwa na maeneo ya kunawia mikono kwa maji tiririka na sabuni.
Share To:

mwangaza wa hbari

Post A Comment: