Na John Mapepele

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema Serikali imedhamiria kufanya kazi kwa pamoja na wadau mbalimbali wa utalii nchini kwa ajili ya kuimarisha mahusiano ya serikali na wadau (Public Private Partnership) ili kufikia kwa haraka lengo la kuwapata watalii milioni tano hatimaye kuchangia kwenye uchumi wa nchi.

Akizungumza kwenye Tamasha la Kwanza la Biashara la Wadau wa Utalii leo, Februari 23, 2023 lililopewa jina la “The Z sumit” ambapo Rais wa Zanzibar, Mhe. Hussein Mwinyi amekuwa Mgeni Rasmi, Mhe. Mchengerwa amesisitiza kuwa dhamira ya serikali kwa sasa ni kuwashirikisha wadau wote kwenye mnyororo wa thamani wa utalii ili kutoa huduma ya kiwango cha kimataifa kitakachowavutia watalii kuja kujionea vivutio mbalimbali vya utalii hapa nchini.

Aidha, amemhakikishia Mhe. Rais Mwinyi kufanya kazi kwa karibu na Waziri anayesimamia sekta ya Utalii kwa upande wa Zanzibar katika kupanga mikakati ya pamoja ya kutangaza vivutio vya utalii ikiwa ni pamoja na kuwaalika watoa huduma za utalii wakubwa duniani ili kutengeneza mnyororo mzuri wa thamani wa utalii.

Amesema kwa ukubwa wa Tanzania na kwa uwingi wa vivutio vilivyopo bado kuna kazi kubwa inayotakiwa kufanywa kwa pamoja baina ya Serikali na wadau ili sekta ya utalii iweze kuchangia kiasi kikubwa kwenye pato la taifa.

“Kwa ukubwa wa nchi yetu na historia ya nchi yetu hatupaswi kuwa nyuma nina imani tuna kazi kubwa ya kufanya kuitangaza nchi yetu, kwani idadi ya watalii wanaoingia nchini bado kwetu ni aibu kubwa katika sekta zetu kwa hiyo tuna kazi kubwa sana ya kufanya kuwakaribisha wageni kutoka nchi mbalimbali duniani .” amesisitiza Mhe. Mchengerwa

Aidha, amefafanua kwamba wakati umefika wa kuainisha vivutio vingine vya utalii kama utalii wa michezo na utamaduni pia kubuni mikakati kabambe ya kidigitali ya kuutangaza utalii kimataifa.

Akitolea mfano amesema nchi ya China hutoa watalii takribani milioni mia moja na hamsini lakini wanaofika Tanzania ni elfu arobaini na tano tu na kusisitiza kuwa vilevile kunahitajika kazi kubwa ya kuboresha miundombinu ya utalii.

Tamasha hili la kwanza la wadau wa utalii limeratibiwa kwa pamoja na kampuni ya Kilifair kutoka Tanzania Bara na ZATI kutoka Zanzibar kwa lengo la kuandaa jukwaa la kuwakusanya wadau mbalimbali wa utalii kuja kubadilishana uzoefu na kufanya biashara, ambapo litakuwa likifanyika kila mwaka.
Share To:

emmanuel mbatilo

Post A Comment: