Na John Mapepele

Waziri mpya wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mohamed Mchengerewa leo. amekutana kwa mara ya kwanza na Menejimenti ya Wizara yake na ametoa miezi miwili kwa watendaji kuleta mapinduzi yanayosubiriwa na watanzania.

Mhe. Mchengerwa amesema haya mara baada ya kuwasili Makao Makuu ya Wizara hiyo Mtumba jijini Dodoma wakati alipoambatana na Katibu Mkuu mpya wa Wizara hiyo Dkt. Hassan Abbasi ambapo amefafanua kuwa yeye kwa kushirikiana na Viongozi wenzake walioteuliwa hivi karibuni atahakikisha wanafanya mabadiliko na mapinduzi makubwa katika sekta ya utalii ili ichangie zaidi uchumi wa nchi.

Baada ya tukio hilo Waziri Mchengerwa amefanya makabidhiano ya ofisi na aliyekuwa Waziri wa Wizara hiyo Balozi Dkt. Pindi Chana.

‘’Tunahifadhi na kutangaza utalii nchini.Lakini pia twende tukadhibiti ujangili tunataka tudhibiti kwelikweli ili kuhakikisha kwamba vitendo vya hovyo hovyo havitokeo. Na mimi kwenye kipindi changu sitataka kusikia vitendo vya hovyo hovyo,’’ amesema Mchengerwa wakati wa makabidhiano hayo.

Aidha, Mchengerwa ameagiza kupatiwa taarifa za idara na taasisi za Wizara ifikapo Jumatatu, Februari, 20, 2023 ili aweze kuzipitia.

‘’Nataka kupitia taatifa hizi halafu tutaitana kwa ajili ya kupanga kazi tuweze kujua ndani ya kipindi cha miezi miwili tumekwendaje kwenye Wizara yetu ili tuweze kutimiza zile ndoto ambazo tunazo za Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan,’’ ameongeza Mchengerwa.

Waziri huyo pia amehimiza ushirikiano baina yake na Waziri aliyekuwepo Balozi Dkt. Pindi Chana. ‘’Naomba sana tushirikiane pale ambapo kuna jambo ambalo mnadhani nahitaji kulipitia wakati wowote . Nitaomba na wengine wakati wowote nitaomba mnipigie kama kuna taarifa ambazo ni za muhimu ili kuboresha zaidi.’’ amesisitiza Mchengerwa.

Katika hafla hiyo pia yamefanyika makabidhiano ya ofisi baina ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Prof.Eliamani Sedoyeka na Katibu Mkuu wa sasa Dkt. Hassan Abbas 
Share To:

emmanuel mbatilo

Post A Comment: