Na. Angela Msimbira OR-TAMISEMI


Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Angellah Kairuki ameagiza Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo kuhakikisha wanaweka utaratibu wa kufanya utafiti wa masomo wanayotoa kama yanatoa tija  kwa wanafunzi na kuwawezesha kutimiza majukumu yao wanapoajiriwa.


Mhe. Kairuki ameyasema hayo leo tarehe 17 Februari, 2023 Jijini Dodoma wakati alipotembelea chuo hicho ikiwa ni utaratibu aliojipangia wa kutembelea taasisi zilizoko chini ya Ofisi ya Rais-TAMISEMI kwa lengo kujionea utekelezaji wa majukumu ya taasisi hizo.


Waziri Kairuki ameendelea kufafanua kuwa chuo hicho kina jukumu la kufanya tafiti za kina kujua wanafunzi wanaomaliza masomo yao wanauwezo wa kutekeleza majukumu  yao  ipasavyo na kuongeza tija katika Halmashauri ili kujiridhisha kuwa mafunzo yanayotolewa yanatija na kuwawezesha kutimiza lile lililokusudiwa na Serikali.


 Amesema kuwa chuo kina jukumu kubwa la kuangalia malengo ya uanzishwaji wake  kwa kuzingatia kuwa Mamlaka za Serikali za Mitaa zinajukumu kufanya kazi kikatiba, kisheria kutokana na majukumu hivyo  Chuo cha Serikali za Mitaa  Hombolo kina jukumu la kuhakikisha wanawajengea uwezo na weledi wanafunzi hao  ili waweze kwenda kuwatumikia wananchi katika Halmashauri hivyo ni muhimu kuangalia kama wanauwezo wa kufanya kazi.


“Wanafunzi wengi wanaomaliza katika chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo  wanategemewa sana kufanya kazi katika Mamlaka za Serikali za Mitaa, hivyo ni jukumu letu kuhakikisha kuwa mafunzo yanayotolewa yanaenda sambamba na matakwa ya Serikali,tuwajengee uwezo, uadilifu na uaminifu katika kutekeleza majukumu yao” amesema Waziri Kairuki


Amesema kuwa Serikali inategemea kuwa na idadi kubwa ya wanafunzi wanaosoma katika chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo wanategemewa kwenda kufanya kazi katika Mamlaka  za Serikali za Mitaa hivyo amewataka kuweka mikakati ya  kuhakikisha tunawajengea uwezo na mbinu za kutimiza majukumu yao


Naye Mwenyekiti wa Bodi  Prof. Joseph amesema chuo hicho kipo katika mkakati wa kutekeleza mpango wa maendeleo  kwa kuboresha miundombinu  ya kufundishia na ujifunzaji  kwa lengo la kuboresha mazingira ya chuo na pia kinaendelea kuwajengea uwezo wafanyakazi  kwa kuwasomesha katika ngazi mbalimbali pamoja  shahada za uzamivu,umahiri na shahada za awali.


Amesema chuo kimeweza kuboresha mifumo ya TEHAMA  na mifumo ya uendeshaji hasa ya kudahili wanafunzi na mifumo ya ukusanyaji wa mapato nia ikiwa ni kuwezesha menejimenti kuweza kusimamia rasilimali zilizopo.


Aidha, amesema chuo kipo katika mkakati wa kuhuisha mitaala ya chuo ili masomo yanayotolewa yaendane  na mahitaji ya soko na kutengeneza programu mpya kwa kuangalia mahitaji.

Share To:

Post A Comment: