Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe.Patrobas Katambi,akijibu swali la msingi la Mbunge wa Kisesa, Mhe. Luhaga Mpina leo Februari 3, 2023 bungeni jijini Dodoma.
........................................

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe.Patrobas Katambi, ametaja mambo sita yanayofanywa na serikali ili kuondokana na tatizo la ajira nchini.

Mhe.Katambi ameyasema hayo leo Februari 3, 2023 bungeni alipokuwa akijibu swali la msingi la Mbunge wa Kisesa, Mhe. Luhaga Mpina.

Katika swali lake, Mbunge huyo amehoji ni vijana wangapi hawana ajira nchini na Serikali imewaandaaje kushindana katika soko la ajira ndani na nje ya nchi.

Akijibu swali hilo, Mhe.Katambi amesema katika kuhakikisha vijana wanaandaliwa ipasavyo kushindana katika soko la ajira la ndani na nje, Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia inatekeleza Mkakati wa Taifa wa Kukuza Ujuzi wa Miaka 10 (2016/2017 –2025/2026).

Amesema kupitia mkakati huo, Serikali imefanya maboresho ya miundombinu na mitaala katika ngazi za Elimu ya Juu, Elimu ya Kati, na Mafunzo ya Ufundi Stadi.

“Aidha, sambamba na maboresho hayo, Serikali inatoa mafunzo ya kuwezesha vijana walio nje ya mfumo rasmi wa mafunzo ili kumudu ushindani katika soko la ajira yakiwemo mafunzo ya uanagenzi,”amesema.

Pia amesema yanatolewa mafunzo ya uzoefu wa kazi kwa wahitimu, mafunzo ya urasimishaji ujuzi uliopatikana nje ya mfumo rasmi wa elimu na mafunzo na mafunzo ya kilimo cha kisasa kwa kutumia teknolojia ya vitalu nyumba.

Awali, amesema utafiti wa watu wenye uwezo wa kufanya kazi wa mwaka 2021 unaonesha kuwa vijana wenye umri wa miaka 15-35 ambao wana ukosefu wa ajira ni 1,732,509.

“Idadi hiyo ni sawa na asilimia 12.2 ya nguvu kazi ya vijana 14,219,191 wenye uwezo wa kufanya kazi kwa maana ya vijana walio katika umri huo na hawapo katika mafunzo au hawana ulemavu unaosababisha wasijishughulishe na shughuli za kiuchumi,”amesema.
Share To:

emmanuel mbatilo

Post A Comment: