Na John Walter-Manyara

Mkuu wa wilaya ya Babati Lazaro Twange amepokea madarasa Manne kati ya 17 yenye thamani ya shilingi milioni 105,351,708.05 yaliyojengwa na MCDO,wananchi wa Sawe pamoja na wadau wengine wa Maendeleo.
Akipokea madarasa hayo mkuu wa wilaya amewashukuru wadau hao kwa uwekezaji huo wenye tija.
Twange amewataka walimu na wanafunzi kuyatunza madarasa hayo na miundo mbinu mingine iliyojengwa shuleni hapo ili yatumike na vizazi vijavyo.
Mkurugenzi wa MCDO Jason Joas Kahembe amesema kwa kushirikiana na Livingstone Tanzania Trust ya Uingereza wamejenga madarasa 14 huku akisema sababu sababu ya Ujenzi huo ni baada ya kupokea maombi kutoka kwa wazazi wa mtaa wa Sawe ili kuwanusuru watoto wao waliokuwa wanatembea umbali mrefu kwenda shule ya Sinai.
Hata hivyo awali MCDO walikuta tayari wananchi wameanza  kujenga madarasa matatu ambayo yalikuwa usawa wa madirisha na mpango wa mradi huo ni kujenga madarasa 17,  bado matatu kukamilisha.
Mwenyekiti wa Halmashauri Abdulrahmani Kololi na Kaimu mkurugenzi wa Halmashauri ya mji wa Babati Anna Fisso wameahidi kufuatilia kwa karibu shule hiyo kuhakikisha samani zote zinatumika ipasavyo kwa wanafunzi hao.
Mbali na madarasa,Pia MCDO katika mradi huo wamejenga ofisi mbili za walimu, ununuzi wa photocopier mashine kwa ajili ya kurahisisha urudufishaji na uchapaji wa mitihani,ununuzi wa vitabu vya kiada kwa madarasa ya 1-7, ujenzi wa vyoo vya wanafunzi na walimu jumla matundu 20, uwekaji wa miundo mbinu ya uvunaji wa maji ya mvua matenki 27 yenye ujazo wa lita 135,000, ununuzi wa kabati 6 na samani zote za shule na ujenzi wa jiko na stoo ya kuhifadhia chakula.
Share To:

Post A Comment: