Na Janeth Raphael

Serikali kupitia Wizara ya Maji imekabidhi magari 10 kwa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kwa ajili ya kuboresha utendaji kazi.

Magari hayo yatagawiwa katika mikoa ya Dodoma, Ruvuma, Rukwa, Morogoro, Iringa, Shinyanga, Mara , Kagera na mikoa iliyopo pembezoni mwa Nchi.

Akizungumza na wandishi wa habari leo Januari 11,2023 Jijini Dodoma, wakati wa kukabidhi magari hayo, Waziri wa Maji Jumaa Aweso amesema changamoto kubwa ambayo husababisha miradi kusuasua ni kutokana na usimamizi na ufuatiliaji.
IMG-20230111-WA0177

Aweso amesema kuwa Rais Samia alianzisha Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) na ndani ya muda mfupi kulikuwa na miradi kichefuchefu zaidi ya 147 lakini ndani ya muda mfupi wameweza kukwamua na kutatua changamoto katika miradi mingi.

“Uanzishwaji wa RUWASA lazima kuwe na vitendea kazi ili kusaidia kusimamia na kufuatilia miradi, leo tumekabidhi magari zaidi ya 10 na haya ni uwezeshaji wa Rais Dk.Samia na tumeshajielekeza kuwa kazi iendelee na hatuna kisingizio.

Na kusisitiza kuwa “”Magari yatumike kwa ajili ya kusimamia miradi ya maji vijijini ili kufanikisha azma ya Rais Dk.Samia ya kumtua mama ndoo kichwani na kufikia asilimia 85 ya upatikanaji wa maji vijijini ifikapo 2025.

Aweso ameagiza kuwa RUWASA wahakikishe magari hayo yanafanya kazi iliyokusudiwa ya kusimamia miradi ya maji kwa weledi.

“Kuwepo kwa vitendea kazi hivi naamini utendaji kazi utaongezeka na kuleta mageuzi na mabadiliko makubwa kwa taasisi hii changa kuendelea kufanya kazi kubwa ya kuwasaidia wananchi kupata huduma ya maji,”amesema Aweso

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa RUWASA Mhandisi Clement Kivegalo amesema mahitaji ya magari kwa wakala huo ni 398 huku yalipo ni 392 ambayo mengi yakiwa katika hali isiyoridhisha kutokana na kutumika kwa muda mrefu.

Amesema kupitia ofisi ya Waziri Mkuu RUWASA ilipata kibali cha kununua magari 123 ambapo kati ya hayo 38 tayari yamepatikana na yapo katika mikoa mbalimbali yakiendelea kutoa huduma.

“Kibali kingine ambacho tumeshatumia ni magari 25 ambapo hayo tumeshalipia ambayo yamegharimu kiasi cha sh.bilioni 3.8, kati ya magari hayo 10 yenye thamani ya sh.bilini 1.5 ndio tumepokea leo na mengine 15 yatafuata,”amesema Kivegalo

Mhandisi Kivegalo amempongeza Rais Samia kwani katika kipindi kifupi ametatua changamoto ya usafiri kwa RUWASA. 

Mhandisi Kivegalo amedokeza kuwa katika mwaka wa fedha ujao Serikali imeahidi kuwanunulia Magari 92 ili kuendeleza kasi ya kuhakikisha wanawahudumia wananchi katika mikoa 25 wanaosimamiwa na RUWASA ukiiondoa Mkoa wa Dar es salaam.
Share To:

Post A Comment: