Serikali mkoani Njombe imekamata nyumba chakavu inayotajwa kutumiwa na mfanyabiashara (jina linahifadhiwa) kwa ajili ya kuchakachua mbolea zikiwemo za ruzuku katika mtaa wa Ramadhani uliopo halmashauri ya mji wa Njombe na kwenda kuwauzia wakulima.

Kamati ya ulinzi na usalama mkoa wa Njombe iliyoongozwa na mkuu wa mkoa huo Anthony Mtaka imefika katika eneo la nyumba hiyo na kukuta shehena ya marobota ya mifuko yenye mbolea na isiyokuwa na mbolea ya ruzuku pamoja na vifaa vingine vinavyotumiwa kwa ajili ya kuchakachua mbolea.

"Tumebaini uwepo wa nyumba ambayo kuna mfanyabiashara anaitumia kuchakachua mbolea,kwa hiyo tumejionea wenyewe marobota ya mifuko yakiwa yametoka kiwandani kwa jina lake na tumekuta nyumba hii haina umeme na jenereta mbili"amesema Mtaka

Mtaka ameongeza kuwa "Nimeelekeza maduka yote ya mfanyabiashara huyu yawekwe chini ya ulinzi na upekuzi ufanyike Nyumbani kwake Ili tujiridhishe kama bidhaa hii ni kwa kiasi gani inafanana na ya dukani kwake na tumewaekekeza mamlaka inayosimamia mbolea waweze kusimamisha leseni ya mfanyabiashara huyu"

Kamanda wa Polisi mkoa wa Njombe Hamis Issah ameihakikishia kamati ya ulinzi na usalama pamoja na wananchi wa mkoa huo kuwa wanakwenda kuweka nguvu ili kuhakikisha jambo hilo linashughulikiwa ili kukomesha swala hilo.



Share To:

Post A Comment: