CHAMA cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Katavi, kimefanya kongamano la kumpongeza Rais Dk Samia Suluhu Hassan kwa kuondoa zuio la mikutano ya hadhara.

Kongamano hilo lililofanyika mjini Mpanda, lilitanguliwa na maandamano yaliyobeba ujumbe wa pongezi kwa Rais Samia kwa hatua yake ya kuruhusu demokrasia kwa vyama vyote vya siasa nchini kufanya mikutano ya hadhara.

Akizungumza katika kongamano hilo, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Katavi, Idd Kimanta amesema hatua hiyo ni busara ya Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, kuruhusu mikutano ya siasa kufanyika bila zuio.

Kutokana na hali hiyo, Kimanta amewataka viongozi na wanachama wa chama hicho mkoani humo kujiandaa kujibu hoja ikitokea zimeibuliwa na vyama vya upinzani kwa njia ya amani na kuendelea kusema mema yaliyofanywa na serikali.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Mrindoko ametoa rai kwa vyama vya siasa kutumia fursa hiyo kunadi sera zao na kufanya siasa za kiungwana, badala ya kutoa lugha za kejeli majukwaani.

Amesema kwa upande wa serikali watasimamia mazingira sawa kwa kila chama kuendesha shughuli zake za kisiasa, ikiwemo mikutano ya hadhara kwa kuweka ulinzi na usalama bila kubagua.

Share To:

Post A Comment: