Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa ameiomba Benki ya Dunia kuwezesha kufanyika kwa tafiti za kina kwa nchi zenye utajiri wa Madini ya Kimkakati  yanayohitajika kwa kiasi kikubwa kwa sasa duniani.


 Amesema  tayari nchi ya Tanzania imekamilisha tafiti za awali kwa madini hayo na kueleza kuwa, inacho kiasi kikubwa cha rasilimali hiyo ikihusisha madini ya Nickeli, Shaba, Cobolt, Vanadium, Kinywe (Graphite) Chuma, Liuthium, Rare Earth Element, Niobium na mengineyo.


Ameongeza kwamba, kutokana na uwepo wa utajiri huo wa kutosha,  bado kunahitajika kufanyika tafiti za  kina na hivyo kuiomba  benki ya dunia  kutoa fedha kwa ajili ya kuendeleza shughuli za utafiti wa madini hayo  ili  kuziwezesha nchi wazalishaji  kujua kiasi kilichopo  cha madini hayo na hatimaye  kuziwezesha nchi hizo kuwa na kanzidata ya madini hayo.


Dkt. Kiruswa ameyasema hayo Januari 10, 2023, wakati akichangia hoja katika Kongamano la Pili la Uendelezaji wa Madini ya Kimkakati unaofanyika katika jiji la Riyadh nchini Saudi Arabia.


Pia, ameiomba benki hiyo kuongeza ushirikiano kwa nchi wazalishaji katika kusaidia kuongeza ujuzi kwa wataalam katika masuala ya utafiti  na uchimbaji wa madini ya kimkakati ambayo ndiyo hitaji kubwa la sasa duniani.


Awali, akifungua mkutano huo, Waziri wa Viwanda na Rasilimali Madini wa Saudi Arabia Mhe. Bandar Ibrahim Al Khorayef ameeleza umuhimu wa nchi za Afrika na Asia kushirikiana katika kusimamia shughuli za utafiti wa madini ya kimkakati ili yaweze kutumika kwa sasa na kuhakikisha yanazinufaisha nchi zenye rasilimali hizo na  kukuza uchumi na maendeleo ya watu.


Kwa upande wake, Balozi wa Tanzania nchini Saudi Arabia Mhe. Jabir Mwadini ameipongeza Wizara kwa kushiriki katika kongamano hilo kutokana na  utajiri wa rasilimali hiyo nchi iliyobarikiwa kuwa nayo ikiwemo madini  hayo inayohitajika  sana kwa sasa duniani na kueleza kuwa, ni fursa muhimu kwa taifa.


Aidha, Mhe. balozi Mwadini ameahidi kuendelea kutafuta wawekezaji ili waweze kuwekeza katika sekta za madini, utalii, uchumi wa buluu na kilimo.


Mkutano huo umehudhuriwa na Mawaziri na wawakilishi kutoka nchi 60 wa wizara za madini za Kanda ya Afrika, Mashariki ya Kati na Asia.


Miongoni mwa masuala muhimu yanayojadiliwa katika kongamano hilo ni pamoja na  namna ya kuzalisha madini hayo pasipo kuchafua mazingira huku rasilimali hiyo ikitakiwa kuzinufaisha kiuchumi nchi wazalishaji.


Kwa upande wa Tanzania, Dkt. Kiruswa ameambatana na  Balozi wa Tanzania nchini humo  Mhe. Ali Mwadini, Kamishna Msaidizi anayeshughulikia masuala ya CSR na  Local Content Maruvoko Msechu na  Mjiolojia kutoka Wizara ya Madini Joseph Ngulumwa.

Share To:

Post A Comment: